Aweso aonya mfumo wa GePG huduma za maji

WAZIRI wa Maji, Jumaa Awesso ameagiza Wakala wa Majisafi na Usafi wa Mazingira (Ruwasa) kuhakikisha Mfumo wa Malipo wa Kielektroniki (GePG) kutokuwa kikwazo cha huduma za maji nchini.

Waziri Aweso ametoa maelekezo hayo wakati akizungumza na kwenye hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi katika mradi wa maji wa Bwanga uliopo wilayani Chato mkoani Geita.

Amesema kwa sasa Jumuiya za Watumuiaji Maji Ngazi ya Jamii (CBWSOs) zimejumuishwa kwenye matumizi ya GePG lakini imebainika zinapata changamoto zinapohitaji pesa ya matengenezo ya dharura.

Amesema lengo la CBWSOs kuunganishwa kwenye GePG ni kuona watu wanaendelee kuchangia na huduma ziendele kuwa bora lakini ni lazima kuwe na utaratibu mzuri pale mifumo inapopata hitilafu.

Waziri Aweso amesema kumekuwepo mlolongo mrefu pale Jumuiya inahitaji kupata pesa ya matengenezo na kulipia gharama za umeme kiasi cha kuathiri muendelezo wa huduma bora za maji safi na salama.

“Katibu mkuu upo, wekeni mfumo rahisi, tunataka pesa ziingie kwenye huo mfumo sawa lakini pale zinapohitajika kwa ajili ya marekebisho ama utoaji wa huduma upatikanaji wake uwe rahisi.

“Tusije tukaweka mifumo badala ya kuleta ahueni, inaleta changamoto na inaleta chuki kwa taasisi, hayo ndiyo maelekezo yafanyiwe kazi wananchi hawa waendelee kunufaika na matunda ya miradi,” amesema.

Meneja wa Ruwasa wilaya ya Chato, Mhandisi Avitus Exavery amesema mradi wa maji Bwanga-Chato unatekelezwa kwa fedha za P4R na utanufaisha vijiji viwili vya Bwanga na Izumangambo.

Amesema zaidi ya watu 27,721 watanufaika na mradi huo unaotekelezwa chini ya mkandarasi Otonde Construction Ltd, kwa mkataba wa Sh bilioni 1.6 na amelipwa Sh bilioni 1.3.

Amesema mradi ulianza kutekelezwa Oktoba 28, 2023 na ulipangwa kukamilika mwezi Juni 2024 lakini mkandarasi ameongezewa muda hadi Oktoba 28, 2024 ili akamilishe usambazaji wa huduma ya maji.

Amesema mradi umefikia asilimia 99, na tayari ujenzi wa tenki la lita 225,000 umekamilika ambapo chanzo cha maji cha mradi ni visima viwili vyenye uwezo wa kuzalisha lita 15,000 kwa saa.

Mbunge wa Jimbo la Chato, Dk Medard Kalemani amesema mpaka sasa Chato ina jumla ya miradi 16 ya maji ambapo mradi wa Bwanga ni miongoni mwa miradi nane mipya ya maji inayotekelezwa.

Mbunge Kalemani amekiri eneo la Bwanga ni miongoni mwa maeneo yaliyokuwa na ukata mkubwa wa maji na sasa mradi umetoa ahueni kubwa kwa wananchi jimboni humo.

Habari Zifananazo

Back to top button