Biashara ya magari yaongeza fursa za kiuchumi

DAR ES SALAAM. Kampuni ya Jan International imesema shughuli zake za biashara ya magari nchini zimeendelea kuchangia shughuli za kiuchumi kupitia ajira, mapato ya Serikali na huduma kwa wateja kutoka maeneo mbalimbali nchini.
Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Ally Akbar, amesema Jan International imekuwa ikifanya biashara Tanzania kwa zaidi ya miaka 15, kipindi ambacho shughuli zake zimehusisha wadau mbalimbali katika sekta ya magari na kutoa fursa za kiuchumi.
Akizungumza katika hafla ya kuwathamini wateja, Akbar amesema shughuli za kampuni hiyo zimechangia ajira katika sekta ya magari, ikiwemo maeneo ya mauzo, huduma kwa wateja na shughuli nyingine za uendeshaji.
Amesema biashara ya magari inaunganisha wadau mbalimbali katika mnyororo wa thamani, wakiwemo wanaojihusisha na usafirishaji, matengenezo ya magari, vipuri na huduma nyingine zinazohitajika na wamiliki wa magari.
“Tumekuwa Tanzania kwa zaidi ya miaka 15. Wateja wetu si wa Dar es Salaam pekee, bali wanatoka katika mikoa mbalimbali na wanaendelea kututembelea kwa ajili ya kununua magari,” amesema.
Akbar amesema kampuni hiyo inaendesha shughuli zake kwa kuzingatia sheria na taratibu za Tanzania, akieleza kuwa uzingatiaji wa sheria ni muhimu katika kujenga mahusiano mazuri na mamlaka pamoja na wateja.
Kuhusu mahusiano na wateja, amesema kampuni imekuwa ikiandaa matukio mbalimbali ya kuwathamini wateja waliodumisha uhusiano wa muda mrefu na kampuni hiyo.
Katika droo ya bahati nasibu iliyofanyika Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, Omar Tajiri ameshinda gari, huku washindi wengine wakipata zawadi mbalimbali zikiwemo pikipiki, simu, televisheni ya inchi 75, Sh19 milioni taslimu, punguzo la asilimia 50, friji na zawadi nyingine.
Akizungumza baada ya kushinda gari hilo, Tajiri amesema amekuwa akifanya biashara na Jan International na kwamba amefurahishwa na ushindi huo.
Kwa upande wake, Recho Manyata, aliyeshinda pikipiki, amesema amefurahishwa na zawadi hiyo na anatarajia kuitumia katika shughuli za biashara na usafiri.
Akbar amesema kampuni hiyo pia inaandaa droo nyingine itakayofanyika Desemba, ambapo washindi wanne watapata magari.
Amesema hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za kampuni kuendeleza ushirikiano na wateja na kujenga mahusiano ya muda mrefu nao.



