Tanzania yafungua milango wawekezaji Finland

DAR ES SALAAM: Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirikisho la Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Deogratius Aloyce Massawe, amewaalika wawekezaji kutoka Finland na maeneo mbalimbali ya Ulaya kuwekeza nchini Tanzania, akisisitiza utayari wa sekta binafsi kushirikiana nao katika kujenga ubia na kuimarisha mahusiano ya kibiashara.
Massawe ametoa mwaliko huo jijini Helsinki, Finland, wakati wa mkutano wa maandalizi kuelekea Jukwaa la Uwekezaji na Biashara kati ya Umoja wa Ulaya na Tanzania (EU–Tanzania Investment and Business Forum 2027).
Amesema sekta binafsi nchini iko tayari kuwaunga mkono wawekezaji, kuwaunganisha na wadau sahihi pamoja na kuwezesha mahusiano na jumuiya ya wafanyabiashara nchini ili kuhakikisha fursa za uwekezaji zinageuka kuwa shughuli halisi za kiuchumi.
Amesisitiza kuwa ushirikiano kati ya sekta binafsi na wawekezaji wa Ulaya ni muhimu katika kuongeza uwekezaji, kupanua biashara na kujenga mahusiano ya muda mrefu yenye manufaa kwa pande zote.
Amesema sekta binafsi ina nafasi muhimu katika kujenga imani kwa mazingira ya uwekezaji Tanzania kupitia mazungumzo ya kisera, utetezi wa mazingira ya biashara yanayotabirika na yenye ushindani, pamoja na kuwaunganisha wawekezaji na washirika wenye uwezo katika sekta binafsi.
Akizungumzia maeneo yenye fursa za uwekezaji, Massawe ametaja kilimo na uchakataji wa mazao, viwanda, madini na uongezaji thamani, pamoja na uchumi wa kidijitali.
Amesisitiza umuhimu wa kuendelea kushughulikia masuala ya kisera na kikanuni yanayoweza kuongeza imani ya wawekezaji na kuwezesha uwekezaji wa muda mrefu nchini.
“Sekta binafsi ya Tanzania iko tayari kuwakaribisha wawekezaji, kujenga ubia na kushirikiana na Serikali katika kushughulikia masuala ya sera na mazingira ya biashara yanayowahusu wawekezaji. Jukumu letu ni kuhakikisha kuwa nia ya kuwekeza inageuka kuwa fursa halisi na endelevu za biashara,” amesema Massawe.
Ushiriki wa TPSF katika mkutano huo ni sehemu ya juhudi za Tanzania za kuimarisha uhusiano wa kibiashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Ulaya kuelekea Jukwaa la Uwekezaji na Biashara kati ya Umoja wa Ulaya na Tanzania la mwaka 2027.



