Bodi ya usajili ya uchukuzi njiani kuanzishwa

DAR ES SALAAM: Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, amesema Serikali itachukua hatua za kuimarisha taaluma ya uchukuzi nchini, ikiwemo kuharakisha mchakato wa kuanzisha Bodi ya Usajili wa Wataalamu wa Uchukuzi, ili kuongeza ubora wa huduma na ufanisi wa sekta hiyo.

Akizungumza wakati wa kufungua kongamano la wataalamu wa usafirishaji na lojistiki lililofanyika katika Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Waziri Mkuu alisema hoja zilizowasilishwa na wataalamu wa sekta hiyo zinaendana na azma ya Serikali ya kuboresha ubora wa huduma katika taasisi za umma.

Aliiagiza Wizara ya Uchukuzi kushirikiana na wadau husika kukamilisha haraka waraka wa Baraza la Mawaziri kuhusu kuanzishwa kwa bodi hiyo ili hatua zinazofuata za utekelezaji ziweze kuanza.

Aidha, alisema Serikali itafanyia kazi mapendekezo ya kuanzisha vitengo maalumu vya usimamizi wa usafirishaji katika wizara, taasisi za umma na halmashauri ili kuboresha matumizi ya rasilimali za Serikali, hususan magari na mifumo ya usafiri.

Katika hotuba yake, Waziri Mkuu alieleza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dk Samia Suluhu Hassan imeendelea kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika miundombinu ya reli, bandari, viwanja vya ndege na usafiri wa majini, hatua zilizochangia kuongeza mchango wa sekta ya uchukuzi katika ukuaji wa uchumi na mapato ya fedha za kigeni.

Alitaja utekelezaji wa Reli ya Kisasa (SGR), maboresho ya Bandari ya Dar es Salaam na bandari nyingine, pamoja na upanuzi wa viwanja vya ndege kuwa miongoni mwa miradi mikubwa inayoboresha ushindani wa Tanzania kama kitovu cha biashara katika ukanda.

Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji, Dk Prosper Mgaya, alisema uwekezaji wa Serikali umewezesha chuo hicho kuanza kutoa mafunzo ya urubani nchini, jambo ambalo hapo awali lilionekana kuwa ndoto.

Alisema tayari wanafunzi 22 wameandikishwa katika programu ya urubani, ambapo wanne wamehitimu na wanane wamefikia hatua ya kuruka ndege peke yao (solo flight), hatua muhimu kabla ya kuhitimu rasmi.

Dk Mgaya alisema hatua hiyo itasaidia kuziba pengo la marubani wazawa, hususan katika Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), ambalo limeongeza idadi ya ndege zake na linahitaji wataalamu wengi zaidi.

Naye Rais wa Chama cha Wataalamu wa Lojistiki na Usafirishaji Tanzania (TANTA), Alphonce Mwingira, alisema sekta ya uchukuzi bado inakabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo kutokuwepo kwa bodi ya usajili wa wataalamu, ukosefu wa vitengo maalumu vya usimamizi wa usafirishaji katika taasisi za umma na kutokuzingatiwa kwa taaluma husika wakati wa matangazo ya ajira.

Alisema matumizi sahihi ya wataalamu wa uchukuzi yanaweza kupunguza gharama za uendeshaji wa shughuli za usafirishaji kwa kati ya asilimia 15 hadi 25 na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi.

Waziri Mkuu aliwahakikishia washiriki wa kongamano hilo kuwa Serikali imezipokea hoja zote zilizowasilishwa na itazifanyia kazi kwa kushirikiana na wizara na taasisi husika, huku akisisitiza kuwa maendeleo ya sekta ya uchukuzi ni msingi muhimu wa kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button