Chunya kukusanya Sh Bil 20 mapato ya ndani

MBEYA; HALMASHAURI ya Wilaya ya Chunya, Mkoani Mbeya inatarajia kukusanya Sh bilioni 20 za mapato ya ndani katika mwaka wa fedha 2026/2027, ikiwa ni ongezeko la Sh bilioni nne kutoka Sh bilioni 16 zilizokusanywa mwaka 2025/2027.
Katika mwaka wa fedha 2025/2026, halmashauri hiyo ilivuka lengo la kukusanya mapoti ya ndani kwa asilimia 126,baada ya kukusanya Sh bilioni 16 dhidi ya lengo la shilingi bilioni 13 zilizokusudiwa,hatua inayofanya Chunya kuwa kinara wa ukusanyaji wa mapato ya ndani Mkoa wa mbeya.
Akizungumza katika mkutano wa Baraza la Madiwani uliofanyika kwa ajili ya kuhitimisha mwaka wa fedha 2025/2026,Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo,Tamin Kambona,amesema ukusanyaji wa mapato ndani ya halmashauri hiyo umekua ukuiongezeka kwa kasi miaka ya karibuni.
Kambona amesema mwaka 2021 Halmashauri hiyo ilikua inakusanya shilingi bilioni nne kwa mwaka ,lakini kiwango kimeendelea kuongezeka hadi kufikia shilingi bilioni 16 kwa mwaka wa fedha 2025/2026.
“Kwa mwaka wa fedha 2026/2027, tunalenga kufikisha makusanyo hayo hadi shilingi bilioni 20,”amesema Kambona.
Amesema halmashauri itayafanyia kazi maelekezo yaliyotolewa na mkuu wa wilaya, ikiwa ni pamoja na kubuni vyanzo vipya vya mapato, akisisitiza kuwa utekelezaji wa miradi ya maendeleo unategemea uwepo wa mapato mazuri ya ndani.

Awali Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Mbaraka Batenga, ameitaka halmashauri hiyo kuendelea kubuni vyanzo vipya vya mapato ili kufikia lengo la shilingi bilioni 20 katika mwaka wa fedha 2026/2027 huku akibainisha kuwa lengo ni kuongeza kiwango cha fedha kinachokwenda kwenye maendeleo kutoka asilimia 60 hadi asilimia 80.
Amesema eneo la ardhi ni miongoni mwa vyanzo vinavyoweza kuongeza mapato, hivyo halmashauri inapaswa kurasimisha na kupima maeneo ya ardhi yaliyopo ndani ya wilaya hiyo ili yaweze kuchangia mapato.
Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Kelvin Nshishi, amesema ili kufikia malengo ya ukusanyaji wa mapato kunahitaji uhusiano mzuri na ushirikiano kati ya madiwani na watendaji wa halmashauri, akisistiza umuhimu wa viongozi hao kushirikiana kudhibiti mianya ya upotevu wa mapato hayo.



