Dk Kijaji akagua miradi Bukoba

BUKOBA: Waziri wa Maliasili na Utalii, Ashatu Kijaji, leo amekagua miradi ya maendeleo katika Manispaa ya Bukoba ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku nne mkoani Kagera.

Katika ziara hiyo, Waziri amekagua miradi mitatu yenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 23.8, ikiwemo ujenzi wa Stendi ya Mabasi ya Kyakailabwa, Soko Kuu la Bukoba pamoja na ofisi mpya za Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba.

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa miradi hiyo, Mhandisi wa mradi huo, Mnyara Mwambungu, amesema ujenzi wa Stendi ya Mabasi ya Kyakailabwa umefikia asilimia 10 ya utekelezaji.

Aidha, amesema mkandarasi amelipwa asilimia 22.2 ya fedha za mkataba na kwa sasa hakuna changamoto yoyote inayokwamisha utekelezaji wa mradi huo, ambao unatarajiwa kukamilika Januari 2027.

Kwa upande wa Soko Kuu la Bukoba, Mhandisi Mwambungu amesema ujenzi umefikia asilimia 50 ya utekelezaji, huku mradi huo ukiwa sehemu ya miradi yenye thamani ya shilingi bilioni 18 inayotekelezwa katika eneo hilo na kuongeza kuwa soko kuu la litakuwa na uwezo wa kuhudumia wafanyabiashara 2,400, vizimba 1,800 pamoja na maegesho ya magari makubwa 32.

Waziri huyo pia amekagua ujenzi wa Ofisi mpya za Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba zenye thamani ya Sh bilioni 5.8. Utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 45, ambapo hadi sasa zaidi ya Sh bilioni 4.5 zimetumika.

Akizungumza baada ya ukaguzi huo, Waziri Dk Kijaji amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Kagera pamoja na watendaji wote kuhakikisha wanamsimamia kwa karibu mkandarasi anayetekeleza mradi wa Stendi ya Kyakailabwa ili akamilishe kazi kwa wakati uliopangwa.

Amesisitiza kuwa hakutakuwa na muda wa nyongeza wa utekelezaji wa mradi huo, akieleza kuwa wananchi wanahitaji huduma na maendeleo kwa wakati.

Vilevile, Waziri ameagiza kuhakikisha kunakuwa na miundombinu bora ya barabara zinazoifikia stendi hiyo ili iweze kutoa huduma kwa ufanisi mara baada ya kukamilika

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button