Haki za watoto magerezani zafuatiliwa

Haki za watoto magerezani zafuatiliwa

NAIBU Kamishna wa Utawala na Rasilimali Watu wa Jeshi la Magereza, Jeremiah Katungu ameliagiza dawati la jinsia ndani ya jeshi hilo kuhakikisha wanafuatilia haki za watoto waliopo magerezani ili kuepusha fedheha na malalamiko kutoka kwa jamii.

Aidha, amelitaka dawati la jinsia ndani ya jeshi hilo kuwachukulia hatua kali wafanyakazi watakaotoa siri za wateja wanaokuja kwa ajili ya kueleza unyanyasaji wa kijinsia iwe kwenye ndoa au ukatili wanaofanyiwa ili kukomesha tabia hiyo.

Alitaka kuangaliwa kwa haki za watoto walio magerezani ili zisikiukwe na watakaoshindwa watachukuliwa hatua.

Advertisement

“Dawati linatakiwa kufuata sheria za watoto na haki zao ili kuhakikisha kama watoto wanapata haki hizo kama inavyostahili, wafuatilie kwa kina ili kuona watoto waliopo gerezani wanapata haki za mtoto anazostahili kupata,” alisema.

Alisema hakuna sababu ya askari anayefanya dawati la jinsia kutoa siri za wateja hata kama anafanyia kazi hiyo nje ya ofisi.

“Mkuu wa dawati la jinsia hapa jeshini nakuagiza kuhakikisha unawachukulia hatua kali wale watakaobainika kutoa siri za wateja, hiyo inachangia kwa kiasi kikubwa jamii kushindwa kuleta matatizo ya unyanyasaji wanayopata katika familia zao,” alisema.

Alisema kuna watu wananyanyasika kwenye ndoa na wanahitaji msaada, lakini wakisikia siri zinatolewa ni vigumu kuleta matatizo yao kwa kuhofia siri zao kutolewa nje.

Pia alisema matukio ya unyanyasaji wa kijinsia bado yapo na kwa mujibu wa takwimu za Jeshi la Polisi, kuanzia Januari hadi Juni 2021 idadi ya waliofanyiwa ukatili ni 15,131.

Alisema Jarida la Afrika linaonesha kuwa asilimia 46 ni watu wanaonyanyasika kwenye ndoa, asilimia 36 wananyanyasika kimwili, asilimia 32 wananyanyasika kisaikolojia na asilimia 13 wananyanyasika kingono.

Alisema matukio haya hayapaswi  kupewa nafasi bali yanapaswa kuchukuliwa hatua kali ili yatokomezwe.

Pai alisema jeshi hilo litawapatia vitendea kazi pamoja na ofisi dawati la jinsia ili waweze kufanya kazi kwa weledi unaotakiwa.

Awali Kamishna Msaidizi wa Magereza, Hassed Mkwanda alitaka dawati hilo kuangalia unyanyasaji pande zote kwa maana ya wanawake na wanaume.

Alipongeza mtandao wa dawati hilo kwa kushirikisha wajumbe kutoka mikoa mbalimbali nchini ili waweze kupata mafunzo.

Mkaguzi Msaidizi wa Magereza, Enock Tarimo ameliomba jeshi hilo kuwasaidia kutatua changamoto ya ofisi na vitendea kazi ambavyo vinahitajika katika utendaji kazi wao.