Jamii yaaswa kuelewa zaidi kuhusu vitiligo

DAR ES SALAAM: MWANZILISHI wa Taasisi ya Beyond Skin Initiative, Clementina Chalamila, amesema bado kuna changamoto kubwa ya uelewa katika jamii kuhusu watu wenye vitiligo, hali inayochangia unyanyapaa na kuwakatisha tamaa wengi katika kufikia ndoto zao.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na Daily News Digital, Clementina amesema baadhi ya watu wenye vitiligo huamua kujificha kutokana na hofu ya kukumbana na mitazamo hasi na ubaguzi kutoka kwa jamii.

Amesema yeye binafsi aliwahi kuathirika kisaikolojia kutokana na maneno na mtazamo wa watu baada ya rangi ya ngozi yake kubadilika. Hata hivyo, baadaye aligundua kuwa thamani ya mtu haipimwi kwa mwonekano wa nje, bali kwa uwezo, tabia na kujiamini kwake.

Katika kuthibitisha kuwa bado jamii ina mtazamo hasi kuhusu vitiligo, Clementina amesimulia kisa chake alipokataliwa na mwalimu mkuu wa shule aliyokuwa akisoma. Amesema tukio hilo lilimfanya ajihisi tofauti na wanafunzi wengine na kumfanya aanze kujificha kwa kuogopa mitazamo ya watu.

Aidha, ameeleza kuwa vitiligo si ugonjwa wa kuambukiza na hauzuii mtu kutimiza ndoto zake. Kutokana na hilo, amewahimiza watu wenye hali hiyo kujikubali, kuacha kujificha na kuishi maisha yao kwa ujasiri na kujiamini.

Pia ametoa wito kwa jamii kuacha kuwabagua au kuwacheka watu wenye vitiligo, badala yake iwape heshima, ushirikiano na nafasi sawa katika nyanja mbalimbali za maisha.

Akizungumzia chanzo cha vitiligo, Clementina amesema hali hiyo inaweza kusababishwa na sababu mbalimbali ikiwemo msongo wa mawazo, majeraha kwenye ngozi na kurithi kutoka kwenye familia.

Amehitimisha kwa kusema kuwa watu wengi wenye vitiligo hukosa fursa mbalimbali, ikiwemo ajira, kutokana na unyanyapaa unaoendelea, huku akieleza kwa sasa amejenga kujiamini na amewataka watu wengine wenye changamoto hiyo kufanya hivyo ili wasiruhusu hali yao iwe kikwazo cha kutimiza malengo yao.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button