JK ataka Afrika iwekeze kwenye elimu

DAR ES SALAAM: Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne wa Tanzania, Dk Jakaya Kikwete, amesema uwekezaji katika elimu bora ndiyo msingi muhimu wa kuwaandaa vijana wa Afrika kwa ajira za baadaye, ujasiriamali na mabadiliko ya kiuchumi.
Akizungumza katika Mkutano Mkuu wa Wanahisa wa Africa50 uliofanyika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam, Dk Kikwete amesema upanuzi wa elimu ya sekondari uliofanyika wakati wa uongozi wake ulilenga kuhakikisha watoto wanaomaliza shule ya msingi wanapata nafasi ya kuendelea na masomo pamoja na kupata ujuzi unaohitajika.
“Nilipoingia madarakani, ni asilimia sita tu ya watoto waliomaliza shule ya msingi waliokuwa wanafanikiwa kuingia sekondari,” alisema.
Alieleza kuwa juhudi za awali zilielekezwa zaidi katika elimu ya msingi kwa wote, jambo lililoongeza uandikishaji hadi zaidi ya asilimia 98 ya watoto wenye umri wa kwenda shule, lakini elimu ya sekondari haikupanuka kwa kasi inayolingana na ongezeko la wanafunzi waliomaliza shule ya msingi.
“Ilitubidi kufanya kazi kubwa kuhakikisha wavulana na wasichana wanaomaliza shule ya msingi na kufaulu mitihani yao wanapata nafasi ya kujiunga na sekondari. Lakini si suala la kuwa shuleni tu, bali ni kupata elimu bora inayowezesha kujifunza kwa ufanisi,” alisema.
Dk Kikwete alisema dhamira hiyo ndiyo inayoendelea kumuongoza katika nafasi yake ya Mwenyekiti wa Bodi ya Global Partnership for Education (GPE), ambako amekuwa akisisitiza kuwa ujenzi wa nguvu kazi yenye tija huanza na elimu imara ya awali, msingi na sekondari.
Alibainisha kuwa watoto milioni 270 duniani kwa sasa wako nje ya mfumo wa elimu, huku milioni 110 kati yao wakiwa barani Afrika.
“Afrika ndiyo Bara lenye idadi kubwa zaidi ya watoto wasiokuwa shuleni. Na hata wale waliopo shuleni, wengi hawamalizi elimu ya msingi au hawapati ujuzi unaotakiwa kulingana na kiwango chao cha elimu,” alisema.
Alihimiza kuimarishwa kwa elimu ya sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati (STEM), kuboreshwa kwa elimu ya ufundi na mafunzo ya ujasiriamali.
“Ajira rasmi pekee haziwezi kuwachukua vijana wote wanaoingia kwenye soko la ajira,” alisema.
Dk Kikwete alikumbusha kuwa alipohitimu chuo kikuu mwaka 1975, waajiri walikuwa wanakwenda vyuoni kuwachukua wahitimu, lakini leo wahitimu wengi wanapata ugumu mkubwa kupata ajira.
“Huo ndiyo ukweli wa sasa. Mafunzo ya ujasiriamali ni muhimu ili vijana waweze kuanzisha biashara zao na kujipatia kipato,” alisema.
Alionya kuwa Afrika inaweza kupoteza fursa zinazohusiana na ajira milioni 230 zinazotarajiwa kuhitaji ujuzi wa kidijitali ifikapo mwaka 2030 endapo mifumo ya elimu haitabadilika kwa kasi inayohitajika.
“Teknolojia inabadilika haraka. Ajira zinatengenezwa, zinabadilishwa na nyingine zinapotea kwa wakati mmoja. Lazima tuwape vijana wetu ujuzi unaohitajika na soko la ajira,” alisema.
Kwa mujibu wa Dk Kikwete, mifumo ya elimu inapaswa kuzalisha watu wenye uwezo wa kufikiri kwa kina, kutatua matatizo, kubuni, kufundisha na kufanya ujasiriamali, huku kujifunza maisha yote na uwezo wa kuendana na mabadiliko vikizidi kuwa muhimu katika uchumi wa kisasa.

Alisema GPE inasaidia nchi zenye kipato cha chini na cha kati, zikiwemo nchi 44 za Afrika, kwa kusaidia kuunganisha maendeleo ya miundombinu ya shule na mipango mipana ya sekta ya elimu.
Msaada huo unahusisha ujenzi na ukarabati wa madarasa, upatikanaji wa maji na huduma za usafi pamoja na mazingira salama na jumuishi ya kujifunzia, hasa kwa wasichana, watoto kutoka mazingira magumu na wanafunzi wenye mahitaji maalumu.
Dk Kikwete alisema GPE imetenga dola za Marekani milioni 329.9 kusaidia kuboresha ubora wa elimu nchini Tanzania tangu mwaka 2019, huku maendeleo ya miundombinu ya shule yakiendelea kuwa kipaumbele kikubwa.
Aliipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuimarisha upatikanaji wa elimu na matokeo ya ujifunzaji.
Alisema katika mwaka mmoja wa fedha wa 2024/25 na 2025/26 pekee, serikali imejenga shule mpya 277 za sekondari, madarasa 2,429 ya shule za msingi, madarasa 930 ya awali na madarasa 64 kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu.



