JKT kuendeleza shamba darasa baada ya Nanenane 2026

DODOMA: JESHI la Kujenga Taifa (JKT) limesema litaendelea kuwa shamba darasa la kilimo, mifugo na uvuvi hata baada ya kufungwa kwa Maonesho ya Nanenane 2026, kwa lengo la kuwajengea wananchi uwezo wa kuongeza tija katika uzalishaji.

Mkuu wa JKT, Meja Jenerali Rajab Mabele alisema hayo alipotembelea banda la jeshi hilo katika Maonesho ya Nanenane yanayoendelea Viwanja vya John Malecela, Nzuguni, jijini Dodoma.
Alisema maonesho hayo si shughuli ya muda mfupi, bali ni sehemu ya jukumu la JKT la kutoa elimu ya vitendo kwa wakulima, wafugaji na wavuvi kupitia wataalamu wa jeshi hilo na taasisi zake, ikiwamo SUMA JKT.
“Maonesho haya kwetu ni endelevu. Hata yakifungwa tutaendelea kuwafundisha Watanzania kilimo bora, ufugaji wa kisasa na uvuvi wenye tija,” alisema.

Alisema huduma hiyo haipo Dodoma pekee, bali inapatikana pia katika maeneo yote yanayofanyika Maonesho ya Nanenane nchini, ikiwamo Arusha, Morogoro, Lindi, Mbeya na Simiyu, ambako wananchi wanaendelea kupata elimu ya uzalishaji katika maeneo madogo yenye matokeo makubwa.

Pia aliwataka wananchi kutembelea banda la JKT kujionea teknolojia mbalimbali za uzalishaji na bidhaa zinazotokana na shughuli za vijana wanaopata mafunzo ndani ya jeshi hilo.

Aidha, Meja Jenerali Mabele alisema JKT linafanya utafiti wa kuanzisha mfumo wa kuwafuatilia vijana wanaohitimu mafunzo ili kufahamu maendeleo yao na kuhakikisha ujuzi wanaoupata unatafsiriwa kuwa ajira, uzalishaji na maendeleo ya kiuchumi.
Pia aliwahakikishia wananchi kuwa uwepo wa wanajeshi katika maonesho hayo ni kwa ajili ya kutoa elimu na huduma, akisisitiza kuwa JKT ni jeshi la wananchi na linaendelea kushiriki katika maendeleo ya taifa.



