Jumuiya za kiraia zatajwa utakatishaji fedha, ugaidi

Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni.

DAR ES SALAAM; SERIKALI imesema baadhi ya jumuiya za kiraia zinatumika kujihusisha au kufanikisha kutendeka kwa makosa ya jinai na vitendo vingine vyenye madhara kwa jamii ikiwemo utakatishaji wa fedha, ugaidi na usafirishaji wa binadamu.

Hayo yamesemwa leo Machi 26, 2024 na Waziri wa Mambo ya Ndani, Hammad Masauni katika uzinduzi wa kampeni ya usajili jumuiya za kiraia iliyofanyika ukumbi wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam.

Amesema miongoni mwa makosa yanayofanywa na baadhi ya jumuiya za kiraia ni utakatishaji wa fedha haramu, ugaidi na ufadhili wa shughuli za kigaidi, usafirishaji haramu wa binadamu, biashara haramu ya silaha na uwepo wa jumuiya za kidini zinazotoa mafundisho potofu na hatarishi kwa usalama wa raia afya ya mwili na akili.

Advertisement

Masauni amesema, kutokana na vitendo hivyo madhara yake ni kuwa Tanzania imetajwa kuwa na udhaifu wa mifumo ya fedha katika taasisi hizo katika ripoti ya Taasisi ya Kimataifa ya ‘Financial Action Task Force’ (FATF) ambayo ilianzishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

“Ripoti hii inaonesha kuwa nchi yetu haina mifumo mizuri ya usimamizi na ufuatiliaji wa mienendo wa jumuiya za kiraia zikiwemo taasisi na madhehebu ya dini.

“Hivyo kutengeneza mazingira rafiki ya taasisi hizo kutumika au kuwa katika hatari ya kutumika katika utakatishaji wa fedha haramu au kufadhili masuala ya ugaidi. Hali hii imesababisha Tanzania kuwekwa katika kundi la nchi zinazohitaji ufuatiliaji wa karibu yaani Enhanced Monitoring (Grey List)….. Hivyo lazima tushirikiane kwa karibu kuondoa hali hii kwenye nchi yetu,” amesema.

Amesema kutokana na Tanzania  kuwekwa kwenye kundi hilo, vyombo vya kimataifa na wadau mbalimbali wa kimataifa wamekuwa wakipewa tahadhari kuhusu udhaifu wa kusimamia jumuiya hizi ambao unaweza kutumika katika masuala ya utakatishaji wa fedha haramu na ufadhili wa ugaidi.

“Hali hii inaweza kuleta madhara ya kuharibu taswira nzuri ya kidiplomasia iliyopo katika nchi yetu,”amesema.

Amesema Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ambayo kupitia Ofisi ya Msajili wa Jumuiya inatekeleza Mpango Kazi wa FATF utakaowezesha serikali kuondolewa kwenye kundi hilo, lakini pia kufanikisha jukumu la kudumisha amani na utulivu.

/* */