Kamachumu Stars bingwa kombe la Mwijage

KAGERA: Timu ya Kamachumu Stars imeibuka bingwa wa mashindano ya Paul Mwijage Cup baada ya kuifunga Kanoni FC kwa bao 1-0 katika mchezo wa fainali na kujinyakulia kitita cha Sh milioni 3.

Mashindano hayo yaliyoshirikisha timu 20 kutoka Tarafa ya Kamachumu, Wilaya ya Muleba, mkoani Kagera, yamekuwa kivutio kwa mamia ya wananchi huku yakitoa fursa kwa vijana kuonyesha vipaji vyao katika soka.

Mashindano hayo yamejenga taswira mpya katika Tarafa ya Kamachumu na Wilaya ya Muleba kwa ujumla, kutokana na kuibua vipaji vya vijana pamoja na kuwaunganisha wananchi kupitia michezo.

Mkurugenzi wa mashindano hayo, Paul Mwijage, amesema lengo kuu la michuano hiyo lilikuwa kuinua vipaji vya vijana na kuwapa fursa ya kuonekana na kupata nafasi ya kucheza katika timu mbalimbali kubwa.

Amesema baadhi ya vijana waliofanya vizuri katika mashindano hayo watapatiwa nafasi ya kushiriki katika michuano mikubwa na kujaribiwa katika timu mbalimbali, ikiwemo Kagera Sugar na Geita Gold.

Mwijage amesema pia wana mpango wa kuunda uongozi na katiba ya Kamachumu FC, timu itakayoundwa na baadhi ya vijana walioshiriki mashindano hayo na kuwa timu ya wananchi wa eneo hilo.

Amesema lengo ni kuipambania timu hiyo ili iweze kupanda madaraja hatua kwa hatua, kuanzia Ligi Daraja la Kwanza hadi kufikia Ligi Kuu Tanzania Bara.

Akizungumza katika fainali hizo, Afisa Mnadhimu wa Mkoa wa Kagera, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Yussuf Daniel, aliyemwakilisha Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Blasius Chatanda, amemshauri Mwijage kuanzisha pia mashindano ya vijana chini ya umri wa miaka 17.

Amesema mashindano ya vijana yataisaidia Kamachumu na Wilaya ya Muleba kwa ujumla kuibua vipaji halisi tangu katika umri mdogo na kuwajengea msingi mzuri wa kisoka.

Aidha, amewataka vijana kujiingiza katika michezo na kujiepusha na matumizi mabaya ya simu, ikiwemo kujihusisha na mitandao mibaya ya kijamii, badala yake kutumia michezo kama njia ya kujiendeleza, kuunganisha jamii na kuonyesha vipaji vyao.

Kwa upande wake, Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM Mkoa wa Kagera, Hamimu Mahmudu, amewashukuru waandaaji wa mashindano hayo kwa kuanzisha fursa inayolenga kukuza vipaji na ajira kwa vijana.

Amesema mashindano hayo yanaweza kusaidia kupata wachezaji wakubwa kutoka Kamachumu, akitolea mfano wachezaji Salum Ahmed Harufani, Adala Ahmedi Harufani, Wile Kamugisha na Didas Zimbiile ambao wamepata nafasi katika soka.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button