Michezo ya Majeshi yafunguliwa Mwanza

MWANZA; Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla, amefungua rasmi mashindano ya Baraza la Michezo ya Majeshi Tanzania (BAMMATA) leo Septemba 21, 2026 Uwanja wa CCM Kirumba mkoani Mwanza.
Mashindano hayo yanayoshirikisha timu za majeshi na vyombo vya ulinzi na usalama kutoka kanda saba, yataendelea hadi Oktoba 5, mwaka huu, yakiwa na kaulimbiu, ‘Tanzania ni yetu sote, tushikamane kwa pamoja kudumisha amani.’
Akizungumza wakati wa ufunguzi huo, Abdulla amesema dhamira ya mashindano hayo si kuimarisha ushindani wa michezo pekee, bali pia kujenga umoja, mshikamano, urafiki na uhusiano meema miongoni mwa vyombo vya ulinzi na usalama.
Amewapongeza viongozi wa vyombo hivyo kwa kuendelea kuthamini michezo kama nyenzo muhimu ya kujenga nidhamu, upendo na mshikamano.

“Natoa wito kwa wananchi tuendelee kuwa wazalendo na kulinda tunu ya amani ya nchi yetu ili kukuza utalii na maendeleo ya sekta mbalimbali zinazogusa maisha ya watu wetu,” amesema.
Amesisitiza umuhimu wa kufanya mazoezi na kuzingatia lishe bora, akieleza kuwa afya ni mtaji muhimu katika kufikia Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050.
“Mashindano haya yanapaswa kuwa mahali pa kuonesha vipaji, nidhamu na uwezo wa kushindana kwa haki. Nawasihi washiriki na waamuzi kuzingatia kanuni na sheria,” amesema.
Kwa upande wake, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Rhimo Nyansaho, amesema mashindano hayo yanaonesha namna serikali inavyoupa umuhimu michezo katika kujenga afya, nidhamu, umoja na mshikamano.
Mkuu wa Majeshi (CD)F Jacob Mkunda, amesema michezo ndani ya vyombo vya ulinzi na usalama si burudani pekee, bali ni sehemu ya maandalizi ya askari katika kutekeleza majukumu yao.
“Michezo siyo burudani tu bali ni maandalizi ya askari katika kuimarisha ulinzi. Ndani ya jeshi sisi kwetu michezo ni sehemu ya kazi,” amesema.

Awali, Mwenyekiti wa BAMMATA, Meja Jenerali Said Hamis Said, amesema wanamichezo watashindana katika michezo mbalimbali ikiwemo soka, mpira wa mikono, kikapu, wavu, riadha, vishale, kulenga shabaha na netiboli.
Amesema washiriki wanatoka kanda saba ambazo ni Ngome, JKT, Magereza, Uhamiaji, Polisi, Zimamoto na Uokoaji, pamoja na Kikosi Maalum cha SMZ.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, CP Salum Hamduni, amesema mashindano hayo yameleta manufaa mbalimbali ikiwemo burudani, kuongeza mzunguko wa fedha, kujenga mshikamano na kukuza utalii wa michezo, huku akiomba Mwanza ipewe nafasi ya kuandaa mashindano hayo mwaka 2027.



