Kamati ya Bunge yaunga mkono uanzishwaji bodi ya wanajiosayansi

MWANZA: Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Subira Mgalu amesema kuwa miongoni mwa masuala ambayo Kamati hiyo itahakikisha inatekeleza ni pamoja na kufanikisha kuanzishwa kwa Bodi ya Usajili wa Wanajiosayansi Tanzania (Tanzania Geoscientists’ Registration Board).
Mgalu ameyasema hayo Jumatatu, Septemba 14, 2026, jijini Mwanza wakati akifungua Mkutano wa Mwaka wa Wajiolojia Tanzania ambapo alishiriki kama mgeni rasmi katika tukio hilo akiambatana na baadhi ya wajumbe wa Kamati hiyo.
Katika hotuba yake ya ufunguzi, Mgalu amesema kuwa kukosekana kwa Bodi ya kusimamia weledi wa kada ya wanajiosayansi kumesababisha uwepo wa vishoka wanaofanya kazi za kijiolojia bila ya kuwa na sifa stahiki hivyo kusababisha hasara kwa wawekezaji na Serikali kwa ujumla.
SOMA: Tanzania, Ghana kushirikiana kuwainua wataalam wa wanajiolojia
“Jambo hili limesababisha kutokukuwepo kwa mfumo thabiti wa kudhibiti maadili, viwango, taaluma, weledi na utaalamu wa wanajiosayansi walio katika utumishi wa umma na katika sekta binafsi nchini” aliongeza Mgalu.

Kuhusiana na uanzishwaji wa Bodi hiyo, Mgalu amesema kuwa, kwa kuzingatia umuhimu wa chombo hicho, Kamati imeamua kuibeba ajenda hiyo na itahakikisha suala hilo linafikiwa tamati kwa mafanikio.
“Ninatambua kuwa changamoto ya kukosekana kwa Bodi ya Usajili wa Wanajiosayansi Tanzania imekuwepo kwa muda mrefu na hatua mbalimbali zimeendelea kuchukuliwa kuhakikisha uwepo wa chombo hichi muhimu. Hata hivyo, leo nipende kuwahakikishia kuwa Mimi na Kamati yangu tutaibeba ajenda hii na tutahakikisha Bodi hii inaanzishwa kwa maslahi ya kada ya jiosayansi na Taifa kwa Ujumla” alisisitiza Mgalu.
Kwa upande wao, Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini walioshiriki Mkutano wa Wajiolojia kwa mwaka 2026 akiwemo Mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Musukuma na mbunge wa Katoro, Kija Ntemi wamesema suala la uanzishwaji wa Bodi ni la msingi watahakikisha wanaibeba ajenda hii kikamilifu.



