Mabonanza ya watumishi yasifiwa kujenga afya

IRINGA: MABONANZA ya michezo kwa watumishi wa taasisi mbalimbali yameelezwa kuwa na nafasi muhimu katika kuimarisha afya ya mwili na akili, kupunguza msongo wa mawazo na kujenga mahusiano mazuri kazini.

Akizungumza baada ya kuhitimishwa kwa bonanza lililofanyika Septemba 5, 2026 katika viwanja vya Chuo Kikuu Mkwawa (MUCE), Iringa, Mhandisi wa Bodi ya Maji Bonde la Rufiji, David Munkyala, alisema michezo imekuwa njia muhimu ya kuwaunganisha watumishi kutoka taasisi mbalimbali.

Alisema bonanza hilo pia limetoa fursa kwa taasisi kutoa elimu kwa washiriki kuhusu huduma na shughuli zao, ikiwemo utunzaji wa rasilimali za maji, uchimbaji wa visima na utoaji wa vibali vya matumizi ya maji.
Kwa upande wake, Novatus Shayoo kutoka Ofisi ya Master J Tailizi, alisema michezo imewapa watumishi nafasi ya kutoka katika mazingira ya kawaida ya ofisi, kupumzika, kufanya mazoezi na kubadilishana uzoefu.

Naye Mratibu wa bonanza hilo, Ramadhan Rashid, alisema michezo inapaswa kupewa nafasi katika maeneo ya kazi kwa kuwa mbali na kuboresha afya, huimarisha mshikamano na kupunguza msongo wa mawazo.

Bonanza hilo lilihusisha michezo zaidi ya nane, ikiwemo mpira wa miguu, volleyball, netiboli, kuvuta kamba na pool table, likiwakutanisha watumishi kutoka taasisi mbalimbali.



