Madaktari wazawa watenganisha mapacha

MADAKTARI bingwa wazawa wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) wamefanikiwa kufanya upasuaji wa kutenganisha mapacha walioungana aina ya parasitic conjoined twins, mmoja wao akiwa hajakua kikamilifu na akimtegemea mwenzake kwa ukuaji na uhai.
Akizungumza baada ya upasuaji huo jijini Dar es Salaam, Bingwa wa Upasuaji wa Watoto wa MNH, Dk Victor Ngotta, alisema mafanikio hayo yametokana na maandalizi ya kina na ushirikiano wa wataalamu kutoka kada mbalimbali za afya.
Amesema hali ya mapacha hao ilikuwa ya kipekee kutokana na mmoja wao kutokuwa amekua kikamilifu na kuwa na mikono, miguu pamoja na sehemu ya kiuno, huku akimtegemea mwili wa pacha mwenzake kwa ukuaji na uhai.“Upasuaji huu ulihitaji maandalizi makubwa na ushirikiano wa wataalamu kutoka kada mbalimbali ili kuhakikisha usalama wa mtoto anayebaki baada ya kutenganishwa,” alisema.
Dk Ngotta amesema aina hiyo ya upasuaji huhitaji maandalizi maalumu kwa kuwa madaktari wanapaswa kutathmini kwa kina muunganiko wa miili ya watoto hao na namna ya kutenganisha sehemu husika bila kuhatarisha maisha ya mtoto anayebaki.
Amesema mafanikio hayo ni hatua muhimu katika kuimarisha huduma za upasuaji wa kibingwa na ubingwa bobezi nchini, hasa kwa wagonjwa wenye hali zinazohitaji utaalamu wa hali ya juu. “Tunapoendelea kupata uzoefu katika kufanya upasuaji wa aina hii, tunajenga uwezo wa wataalamu wetu na kuongeza nafasi ya wagonjwa wenye changamoto ngumu kupata matibabu hapa nchini,” alisema.
Baada ya upasuaji huo, Dk Ngotta amesema mtoto anaendelea vizuri na anaendelea kuwekwa chini ya uangalizi wa karibu wa madaktari na wataalamu wengine wa afya. Mafanikio hayo yanaongeza ushahidi wa uwezo wa wataalamu wazawa katika kushughulikia matibabu ya kibingwa na ubingwa bobezi, huku yakitoa fursa kwa wagonjwa wenye mahitaji maalumu kupata huduma za matibabu ndani ya nchi.
Upasuaji huo ni miongoni mwa hatua zinazodhihirisha kuongezeka kwa uwezo wa wataalamu wazawa katika kufanya matibabu ya kesi ngumu na adimu zinazohitaji utaalamu wa hali ya juu.SOMA: Bingwa wa tiba ya watoto anayeipaisha Tanzania



