Majaliwa ataka wananchi kupewa muda
Mabwawa, skimu za kisasa kujengwa Mbarali

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa ameagiza wananchi kupewa muda wa kumalizia shughuli zao za Kilimo kabla ya kuondolewa katika eneo maalum lililotengwa kujengwa mabwawa na skimu za kisasa Mbarari mkoani Mbeya.
Majaliwa ametoa agizo hilo leo Januari 17,2023 katika ziara yake na kamati ya mawaziri nane wa kisekta na Wananchi wa eneo la Kapunga-Mbarali Mbeya.

Amesema, Wizara ya Kilimo inapaswa kuhakikisha inawapanga wakulima vizuri na kuweka miundombinu ya umwagiliaji ili wakulima waweze kufanya kilimo cha uhakika.
Awali, akizungumza katika ziara hiyo, Naibu Waziri wa Kilimo, Anthony Mavunde alisema serikali kupitia Wizara ya Kilimo inatarajia kujenga mabwawa makubwa sita na Skimu za umwagiliaji za kisasa nane kwenye eneo la ekari 91,231 lililotengwa kwa ajili ya kilimo Wilayani Mbarali,mkoani Mbeya.

Alisema, lengo ni kukuza Sekta ya Kilimo kwa asilima 10 ifikapo mwaka 2030.
Alimesema baada ya maboresho ya Mpaka wenye tangazo la serikali GN 28 ya kuangalia upya mipaka yake ambayo itaenda kutengeneza eneo la zaidi ya ekari 91,231 kwajili ya Kilimo, Wizara itakuwa na kazi ya kuwapanga wakulima vizuri kwenye maeneo hayo na kujenga Mabwawa na skimu za kisasa
Pia, ujenzi wa miundombinu hiyo ya Kilimo cha umwagiliaji itasaidia kuwa maji yanarudi mtoni kwenye njia yake ya asili na hivyo kuchangia katika uwekezaji mkubwa wa mradi wa kufua umeme wa Bwawa La Nyerere

“Hata hivyo Wizara ya Kilimo kwa kufuata maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan itaweka mfumo wa Mashamba Makubwa (Block Farming System) kwenye maeneo hayo.” Amesema Mavunde
Aidha, amesema hatua inayofuata ni uwekaji wa miundombini rafiki kwajili ya Mifugo katika Mabwawa 14 nchini, ambayo mabwawa hayo yatakuwa na uwezo wa kuhifadhi maji Lita za ujazo 131, 535,000, na kuondoa adha ya mifugo kukosa maji hivyo kutatua migogoro ya wakulima na wafugaji nchini.
Naye Waziri wa Ardhi Dkt. Angeline Mabula ambaye alisema kuwa serikali itachukua hatua za makusudi za kupima maeneo hayo na kuwapatia hati miliki wananchi hao kwa mujibu wa sheria ya ardhi ili kupunguza migogoro isiyo ya lazima.




