WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk Doroth Gwajima amezitaka kampuni binafsi kusaidia kundi la wanawake kiuchumi.
Dk Gwajima alitoa mwito huo jana alipohudhuria mafunzo ya ujasiriamali yaliyotolewa na Taasisi ya Ustawi wa Jamii na kufadhiliwa na Kampuni ya Cocacola Kwanza.
Mafunzo hayo yaliambatana na makabidhiano ya vitendea kazi kwa mamalishe kutoka wilaya za Kigamboni, Kinondoni na Temeke mkoani Dar es Salaam.
Gwajima alisema Rais Samia Suluhu Hassan anathamini kundi hilo ndiyo maana aliliundia wizara yake nao wamuunge mkono kwa kuwa wabunifu kibiashara na kutoa huduma bora kwa wateja.
“Mkafanye biashara kisasa kwa kuwa mna vitendea kazi vya kisasa, msifanye biashara kimazoea,” alisema.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Cocacola Kwanza, Uukungu Sulay, akikabidhi mitungi ya gesi 120, majiko ya gesi 12O na madawati 120 kwa ajili ya wateja watakaotumia huduma ya chakula katika migahawa ya mamalishe hao alisema wanaofa fahario kusaidia kundi hilo.
“Tumewiwa kusaidia kundi hili baada ya Rais(Samia) kulitambua rasmi, tukaona tufanye kitu chenye manufaa ndiyo maana tulianza na kuwapa mafunzo ya utunzaji kumbukumbu, utafutaji masoko na huduma kwa wateja,”alisema Sulay.
“Ni matumaini yetu hiki kidogo tulichowapa kitazalisha mawaziri na wakurugenzi kwani hata mimi ni zao la mchuuzi mdogo kwa maana ya mama yangu alinisomesha kwa kuuza vitu vidogo vidogo,”alisema.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Wamachinga Wilaya ya Temeke, Hashim Mkweche aliwataka mamalishe hao kuingia kwenye mfumo wa kanzidata ili waweze kufikiwa na fursa kutoka serikalini.
“Kwa sasa Wizara inaimarisha mfumo wa kanzidata ambapo wote mnapaswa kujisajili na hili ni agizo la Rais(Samia) ili anapohitaji kutusaidia ajuwe tupo wangapi lakini tusifanye biashara holela na katika maeneo hatarishi, badala yake tufanye katika maeneo rasmi,” alisema.