Mpango aagiza ujenzi soko la kisasa Igunga

Makamu wa Rais Dk Philip Mpango akpokelewa wilayani Igunga kuanza ziara ya kikazi mkoani Tabora leo Oktoba 8.

MAKAMU wa Rais Dkt. Philip Mpango ameiagiza Ofisi ya Rais – TAMISEMI kushughulikia ujenzi wa soko la kisasa la kituo cha mabasi cha Wilaya ya Igunga kutokana na mahitajio ya wananchi.

Dk Mpango ametoa agizo hilo leo Septemba 8 katika Wilaya ya Igunga wakati akianza ziara ya kikazi ya siku nne mkoani Tabora ambapo amezungumza na wananchi waliojitokeza kumpokea katika eneo la barabara ya Mwanzugi wilayani humo..

SOMA: Dk Mpango asisitiza elimu kuepuka maradhi

Advertisement

Pia amesema kutokana na upungufu wa watumishi katika katika sekta mbalimbali wilayani humo, TAMISEMI inapaswa kutoa kipaumbele kwa wilaya hiyo wakati wa upangaji wa watumishi.

Aidha Makamu wa Rais amewasihi wananchi wa maeneo hayo kuweka mkazo katika kuhakikisha watoto wanapata elimu mashuleni badala ya kuwaruhusu kushiriki katika shughuli za uchimbaji wa madini migodini.

Vilevile Makamu wa Rais amewataka viongozi hususani wabunge wa maeneo hayo kuendelea kutoa elimu na hamasa ya mitungi ya gesi ili kwa wananchi ili kuchagiza azma ya matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa lengo la uhifadhi wa mazingira na afya za wananchi.

Makamu wa Rais amewapongeza wananchi wa Igunga kwa kufanya kazi kwa bidii na kuwa wazalishaji wazuri na muhimu wa mazao ya chakula,biashara pamoja na ufugaji.

Amesema serikali itaendelea kuboresha huduma za kijamii katika Wilaya hiyo zikiwemo huduma za maji, elimu, afya na miundombinu ili kurahisisha shuguli za kiuchumi wilayani humo.

Makamu wa Rais amewahimiza wananchi wa Wilaya ya Igunga kujitokeza katika kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika mwezi Novemba 2024 ili kuchagua viongozi bora watakaoshirikiana na wananchi katika shughuli za maendeleo.