KIGOMA: MAKAMU wa Rais Dkt. Philip Mpango amesisitiza umuhimu wa wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii kuwasaidia wananchi kwa kutoa elimu kuepukana na maradhi mbalimbali.
Ametoa wito huo mara baada ya kutembelea Zahanati ya Kijiji cha Kasumo akiwa wilayani Buhigwe mkoani Kigoma.
Amesema maradhi yanayotajwa kuwasumbua wananchi wa kijiji hicho ikiwemo magonjwa ya mfumo wa hewa pamoja na yanayokana na matumizi ya maji yasio salama yanaweza kudhibitiwa kwa kutoa elimu kupitia mikutano mbalimbali ya kijiji.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii Januari 31, 2024 Dar es Salaam Waziri wa Afya Ummy Mwalimu alisema wahudumu hao ndio Mstari wa mbele katika Sekta ya Afya wanaoweza kuibua wagonjwa na kutoa taarifa zote kuhusu masuala ya Magonjwa ikiwemo yasiyoambukiza na yakuambukiza kama ya milipuko.
”Wahudumu wa Afya ngazi ya jamii ndio askari wa mbele katika Sekta ya Afya na ndio wanaibua wagonjwa na wanaweza wakazuia na kutoa taarifa zote kuhusu masuala ya magonjwa na ni nguzo muhimu katika kuimarisha mifumo ya Afya ngazi ya jamii ili kufikia lengo la huduma za Afya kwa wote.” Amesema Waziri Ummy
Aidha, Waziri Ummy alisema Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii wanaenda kuwapunguzia mzigo watumishi katika ngazi za Hospitali kwa kuwa kuna baadhi ya vijiji havina vituo vya Afya au vinapatikana mbali na makazi ya watu.
“Ndio maana tumeona ni muhimu sasa turasimishe mpango huu ili kutomuacha mtu yoyote, Mfano kwa upande wa ugonjwa wa Kifua Kikuu tulipoamua kutumia wahudumu wa Afya ngazi ya jamii wameibua wagonjwa wapya asilimia 50 kwa kila wagonjwa wapya 100 wanaogunduliwa na ugonjwa huo.” Amesema Waziri Ummy