Wizara yaja na vipaumbele 8 bajeti 2026/27

DODOMA; WIZARA ya Mambo ya Ndani ya Nchi itatekeleza maeneo nane ya vipaumbele katika bajeti ya Mwaka wa Fedha 2026/27.
Akiwasilisha bajeti hiyo bungeni leo, Waziri wa mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi ametaja kuwa ni kuendelea kuboresha miundombinu ya vyombo vya usalama chini ya wizara ikiwa ni pamoja na makazi ya maofisa, wakaguzi, askari na watumishi wasio askari.
“Kuendelea kuboresha upatikanaji wa vitendea kazi ikiwemo vyombo vya usafiri na usafirishaji kwa vyombo vya usalama vilivyopo chini ya Wizara.
“Kuendelea kufanya tafiti mbalimbali ili kubaini sababu za makosa mapya na kuweka mikakati ya kukabiliana nayo.
“Kuendelea kuboresha matumizi ya TEHAMA katika huduma zinazotolewa na wizara pamoja na vyombo vyake; kuendelea kuwajengea uwezo watumishi na askari kwa kuwapatia mafunzo mbalimbali ili kuwaongezea weledi katika utekelezaji wa majukumu yao;
“Kuanza ujenzi wa ofisi ya makao makuu ya NIDA jijini Dodoma na ofisi 31 za usajili za wilaya pamoja na kituo cha mafunzo na matengenezo ya vifaa vya TEHAMA Kibaha; kuanza ujenzi wa nyumba salama kwa ajili ya waathirika wa usafirishaji haramu wa binadamu jijini Dar es Salaam.
“Kuimarisha shughuli za uzalishaji mali kupitia kilimo, mifugo na viwanda pamoja na utunzaji wa mazingira,” amesema Waziri Katambi.



