Benki ya TADB yapewa tuzo

DAR ES SALAAM; Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imetunukiwa Tuzo ya Benki Bora katika Kutoa Suluhisho za Ufadhili wa Kilimo nchini Tanzania, iliyotolewa na Global Brand Awards.
Taarifa iliyotolewa na benki hiyo Julai 31, 2026 imeeleza tuzo hiyo ni uthibitisho wa dhamira yake ya kuendelea kutoa suluhisho bunifu za kifedha zinazochochea maendeleo ya sekta ya kilimo, kuwawezesha wakulima na wadau wote wa mnyororo wa thamani wa kilimo, pamoja na kuimarisha usalama wa chakula na ukuaji wa uchumi wa taifa.
“Aidha, tuzo hii inadhihirisha nafasi ya TADB kama benki ya maendeleo barani Afrika inayoibuka kwa ubunifu katika utoaji wa suluhisho za ufadhili wa kilimo na mikopo ya kijani (Green Finance), inayochochea uwekezaji endelevu na ustahimilivu wa sekta ya kilimo dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi.
“Tunatoa shukrani za dhati kwa wateja wetu, Serikali, washirika wa maendeleo, wadau wetu wote na wafanyakazi wa TADB kwa ushirikiano wao, imani waliyoendelea kutuonyesha na mchango wao katika kufanikisha mafanikio haya.
Mafanikio haya yanatupa ari na nguvu mpya ya kuendelea kuchagiza maendeleo ya sekta ya kilimo kupitia suluhisho za kifedha zenye tija, bunifu na endelevu kwa ustawi wa Watanzania,”imesema taarifa hiyo.



