Mradi milki za ardhi kuajiri 10,000

SERIKALI imesema inatarajiwa mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi nchini (LTIP) kutoa ajira zaidi ya 10,000 na ujuzi wa ziada kwa watu zaidi ya milioni 1.6.

Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Ridhiwani Kikwete alisema Dodoma jana kuwa mkataba wa makubaliano ya utekelezaji mradi huo ulisainiwa na Serikali ya Tanzania na Benki ya Dunia (WB) Februari mwaka jana na utatekelezwa kwa miaka mitano (Julai 2022 hadi Juni 2027).

Waziri Ridhiwani alisema hayo wakati akifungua mkutano wa kitaifa wa wadau wa miradi wa uboreshaji wa usalama wa milki za ardhi.

Advertisement

Alisema mradi huo utakaogharimu dola za Marekani milioni 150 sawa na takribani Sh bilioni 345 na utatekelezwa nchini katika mikoa 16 kwenye halmashauri 41 na kwa wastani wa asilimia 80 utatekelezwa na sekta binafsi, mashirika yasiyo ya serikali na ya kijamii.

Ridhiwani alisema kampuni binafsi zitatekeleza kazi za urasimishaji ardhi mijini kwa asilimia 80, urasimishaji vijijini utatekelezwa na mashirika yasiyo ya kiserikali na mashirika ya kijamii kwa asilimia 60 na ujenzi wa majengo mbalimbali utafanywa na kampuni binafsi kwa asilimia 100 kipaumbele kikiwa kampuni za wazawa.

Alisema sehemu kubwa ya fedha za mradi huo zitatumika kupitia sekta binafsi kwa kuwa hakuna kipengele cha ajira moja kwa moja ila ajira za Watanzania zitatokana na kampuni na mashirika yatakayoshiriki katika utekelezaji wa mradi.

Mradi huo unalenga kuboresha usalama wa milki za ardhi kwa kupanga, kupima na kusajili milki za ardhi zipatazo milioni 2.5 zinazojumuisha hati milki 1,000,000 na leseni za makazi 1,000,000 katika maeneo ya mijini na hati za hakimilki za kimila 500,000 vijijini.

Pamoja na kupima na kutambua vipande vya ardhi yakiwamo mashamba na makazi pia utatoa hatimilki, utasimika mfumo unganishi wa kielektroniki wa kuhifadhi kumbukumbu za ardhi (ILMIS) katika ofisi za ardhi za mikoa na ofisi za halmashauri 41 zinazokarabatiwa.

Ofisi hizo zitaunganishwa na mfumo wa kielektroniki wa usimamizi wa ardhi, kujenga mfumo wa kielektroniki wa thamani za ardhi, kujenga miundombinu ya taarifa za kijiografia pamoja na uzalishaji wa ramani za msingi.

Mradi huo utatekelezwa katika mikoa ya Pwani, Simiyu, Iringa, Tanga, Tabora, Geita, Kigoma, Mara, Shinyanga, Dodoma, Mbeya, Kilimanjaro, Ruvuma, Songwe, Katavi na Arusha yenye jumla ya halmashauri 41.

Ridhiwani aliwaagiza wakuu wa mikoa 25 ukiacha wa Dar es Salaam ambao una jengo lenye mifumo ya ILMIS, kusimamia ujenzi wa majengo ya ofisi za ardhi za mikoa wasiwaachie wajenzi peke yao.

Alisema mradi huo ni wa kwanza kwa ukubwa katika sekta ya ardhi kuwezeshwa na Benki ya Dunia kwa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Alisema mradi huo utatumiwa na benki hiyo kupima si tu uwezo wa Watanzania kusimamia na kutekeleza miradi mikubwa ya sekta ya ardhi kwa manufaa ya wananchi na taifa kwa ujumla, bali pia utatumika kupima uwezo wa nchi za Afrika kutekeleza miradi mikubwa kwenye sekta ya ardhi.

Alisema serikali imewaamini sekta binafsi na nia yake ni kuiwezesha na kuijengea uwezo katika masuala ya uendelezaji ardhi, hivyo aliitaka kuonesha ushirikiano na sekta ya ardhi na kuithibitishia dunia kuwa Tanzania inaweza.

Mwakilishi wa Benki ya Dunia, Nicholas Ole Soikan alisema katika utekelezaji wa mradi huo, sekta binafsi inatakiwa kuwapa nafasi vijana, wanawake na watu wenye ulemavu na wa pembezoni.

Alizitaka asasi zitakazoshiriki katika mradi huo, kufanya vizuri ili kuipa sifa Tanzania ili kuwa mfano wa nchi nyingine barani Afrika kujifunza.