Ngajilo aja na mpango wa kuirudisha Iringa Ligi Kuu

IRINGA: Miaka sita tangu Lipuli FC ilipoaga Ligi Kuu Tanzania Bara mwishoni mwa msimu wa 2019/20, Mkoa wa Iringa unaonekana kuanza safari mpya ya kutafuta nafasi yake tena kwenye ramani ya soka la juu nchini.

Kushuka daraja kwa Lipuli, kufuatia matokeo yasiyoridhisha yaliyoambatana na changamoto za kiuchumi na uendeshaji wa klabu, kuliacha pengo kubwa kwa mashabiki wa soka wa mkoa huo ambao hadi leo wameendelea kutamani kuona timu yao ikirejea katika jukwaa la juu la soka Tanzania.

Sasa matumaini hayo yameanza kupata uhai mpya baada ya Mbunge wa Iringa Mjini, Fadhili Ngajilo, kutoa wito wa kuunganisha nguvu za wananchi, wafanyabiashara, wadau wa michezo na wazawa wa Iringa waliopo ndani na nje ya mkoa ili kuanzisha mpango wa muda mrefu wa kuijenga timu itakayopanda na kudumu katika Ligi Kuu Tanzania Bara.

Akizungumza katika Uwanja wa Samora wakati akikabidhi vifaa vya michezo kwa timu 16 zilizofuzu hatua ya 16 bora ya Ngajilo Super League 2026, Ngajilo alisema Iringa imefika mahali ambapo inapaswa kuacha mazungumzo na kuanza utekelezaji wa ndoto ya kuwa na timu yake ya Ligi Kuu.

Alisema mafanikio ya Ngajilo Super League, iliyoanzishwa mwaka 2010 na sasa ikiwa imetimiza miaka 15, yanaonyesha kuwa Iringa ina hazina kubwa ya vipaji vya soka pamoja na ushindani wa kutosha. Kilichobaki ni kujenga mfumo imara wa uongozi na fedha utakaoiwezesha timu kushindana kwa mafanikio.

“Iringa imekuwa ikizungumza kwa muda mrefu kuhusu kuwa na timu ya Ligi Kuu. Sasa ni wakati wa kubadili nadharia hiyo kuwa uhalisia. Tunahitaji timu itakayobeba heshima ya mkoa wetu na kuitangaza Tanzania nzima,” alisema Ngajilo.

Alisisitiza kuwa timu hiyo haitakuwa ya Iringa Mjini pekee, wala ya wilaya moja, bali ya Mkoa mzima wa Iringa huku akiwataka wananchi wa Kilolo, Mufindi, Kalenga, Isimani na Iringa Mjini, pamoja na wazawa wanaoishi Dar es Salaam, Dodoma, Mbeya, Njombe na maeneo mengine nchini, kuwa sehemu ya safari hiyo.

Kwa mujibu wa Ngajilo, changamoto kubwa si kununua au kuanzisha timu, bali kuhakikisha inakuwa na uwezo wa kujiendesha kwa misingi ya kitaalamu na kifedha.

Alipendekeza kuanzishwa kwa mfuko maalumu utakaotegemea mfumo wa kisasa wa uanachama na uchangiaji wa fedha kwa njia za kidijitali.

Alisema hata michango ya Sh 1,000 kwa mwezi kutoka kwa maelfu ya wananchi inaweza kuwa mtaji mkubwa wa kugharamia mishahara ya wachezaji, maandalizi ya timu, safari, malazi na shughuli nyingine za uendeshaji wa klabu.

Mbunge huyo pia alipendekeza kuundwa kwa kamati maalumu ya fedha itakayohakikisha michango yote inakusanywa na kutumika kwa uwazi na uwajibikaji, akisisitiza kuwa mafanikio ya klabu yoyote ya kisasa huanza na utawala bora kabla ya mafanikio ndani ya uwanja.

Aidha, aliwataka wadau mbalimbali kujitokeza kuunga mkono Ngajilo Super League ili maendeleo ya soka la Iringa yasiendelee kutegemea mfadhili mmoja, akisema ushirikiano mpana ndiyo msingi wa kujenga timu yenye ushindani wa kudumu.

Katibu wa Chama cha Soka Wilaya ya Iringa (IDFA), Yahaya Mpelembwa, alisema uwekezaji wa Ngajilo umeifanya ligi hiyo kukua kutoka mashindano ya Manispaa ya Iringa hadi kuwa mashindano yanayoshirikisha timu kutoka majimbo ya Iringa Mjini, Isimani na Kalenga.

Alisema timu 16 zilizofuzu hatua ya 16 bora zimepitia ushindani mkubwa na sasa zitaingia hatua ya mtoano kutafuta bingwa atakayewakilisha Wilaya ya Iringa katika mashindano ya ngazi ya mkoa.

Naye Mwenyekiti wa IDFA, Joel Musiba, alisema Ngajilo ameendelea kuwa mdhamini mkuu wa ligi hiyo kwa zaidi ya misimu mitano mfululizo, hatua iliyosaidia kuongeza ushindani na kuinua kiwango cha soka katika wilaya hiyo.

Musiba alisema IDFA itaendelea kushirikiana na wadau wote wanaolenga kuendeleza mchezo huo bila kujali tofauti zao, huku akiwasihi viongozi wa timu kuthamini mchango wa wadhamini kwa kutekeleza masharti ya mashindano, ikiwemo matumizi ya jezi zenye nembo ya mdhamini rasmi.

Pia alimuomba Ngajilo kuendelea kuisaidia timu itakayotwaa ubingwa wa Ngajilo Super League katika safari yake ya mashindano ya ngazi ya mkoa, akieleza kuwa mafanikio hayo yanaweza kuwa mwanzo wa safari ya Iringa kurejesha timu yake katika Ligi Kuu Tanzania Bara.

Habari Zifananazo

One Comment

  1. Google is now paying $300 to $500 per hour for doing work online work from home. Last paycheck of me said that $20537 from this easy and simple job. Its amazing and earns are awesome. No boss, full time freedom and earnings are in front of you. This job is just awesome. Every person can makes income online with google easily…………
    .
    M­­­­­­o­­­­­­r­­­­­­e­ D­­­­­­e­­­­­­t­­­­­­a­­­­­­i­­­­­­l­­­­­­s For Us→→→→ https://Www.Payathome9.Com

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button