Nyang’hwale wafikia 61% upandaji miti

HALMASHAURI ya Wilaya ya Nyang’hwale mkoani Geita imefanikiwa kupanda jumla ya miti 926,944 kwa mwaka wa fedha 2023/24 sawa na asilimia 61.79 ya lengo la kupanda miti milioni 1.5 kila mwaka.

Halmashauri imetekeleza mradi huo kwa kushirikiana na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) na wadau wa mazingira ikiwemo RIHEO ambapo kiwango cha kuishi cha miti hiyo ilikuwa asilimia 85.

Advertisement

Ofisa Misitu Wilaya ya Nyang’hwale, Mrema Juma amesema hayo mbele ya viongozi wa mbio za mwenge walipotembelea mradi wa Upandaji miti katika Shule ya Sekondari Igalula Mining.

Mrema amesema mradi wa miti shuleni hapo ulianza Novemba 2023 kutokana na miche vilivyozalishwa kwenye vitalu vya mashuleni ambapo idadi ya miti iliyozalishwa na kupandwa ni miti 643.

Ameainisha kuwa miti iliyopandwa imegawanyika katika makundi mawili ambapo ipo miti ya kivuli pamoja na miti ya matunda kwa mchanganyiko tofauti.

Amesema: “ni kulinda majengo ya shule dhidi ya majanga yatokanayo na upepo mkali, Kuleta kivuli na hewa safi kwa ajili ya mapumziko ya wanafunzi, Kuboresha lishe ya wanafunzi kutokana na ulaji wa matunda.

“Miti hii imepandwa katika maeneo ya Taasisi za Serikali kama shule, zahanati, vituo vya afya, ofisi za kata na ofisi za ngazi ya wilaya na maeneo ya Wananchi.

“Kwa mwaka wa fedha 2023/2024 Halmashauri haikufika Lengo la upandaji wa miti millioni 1.5 kutokana na kukosekana kwa miche kwa wakati.

“Ili kukabiliana na changamoto hii halmashauri inamkakati wa kuanzisha vitalu viwili vya miti kwa fedha za CSR na “Forest Fund” ili kuhakikisha mwaka 2024/2025 tunafikia lengo la kupanda miti milioni 1.5.”

Naye Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa mwaka 2024, Godfrey Mzava amesema ipo haja kwa halamshauri kuwekeza nguvu ya ziada katika upandaji miti kwani Tahari ni imeathirika na mabadiliko ya tabia ya nchi.

“Kwa hiyo mkuu wa wilaya hiyo kampeni lazima iwe ni ya kudumu, na iendelee kusimamiwa wakati wote, kwa ajili ya kupata tija na usalama kwenye mazingira yetu kwa ajili yetu sisi wenyewe na kwa ajili ya vizazi vijavyo,” amesema.