Polisi: Majirani jengeni utamaduni wa kutambuana

MOROGORO; Watanzania wameombwa kujenga utamaduni wa watu majirani kutambuana na inapotokea jirani yako humuelewi vizuri toa taarifa mapema kwa viongozi wa serikali ya mtaa au polisi.
Kauli hiyo imetolewa leo Agosti 27, 2026 na Kamishna wa Polisi Jamii Tanzania, Alex Mkama alipozungumza na waandishi wa habari baada ya kukagua Banda la Polisi Jamii katika Tamasha la Nne la Kitaifa la Utamaduni linalofanyika mkoani Mororgoro na kueleza kwa njia hiyo itasaidia kupunguza baadhi ya vitendo vya jinai.
Pia ametaka jamii itilie mkazo suala la maadili kuanzia ngazi ya familia, kwani maadili ndio yanayofanya watu wawajibike, wachukie rushwa na kuupuka vitendo vya uhalifu.

Ameitaka jamii kujenga tabia ya kutambua majirani zao na pale wanapoona wageni wanaowatilia mashaka watoe taarifa polisi au kwa viongozi wa serikali..
Kwa upande wake Mrakibu Mwandamizi wa Polisi kutoka Makao Makuu ya Jeshi la Polisi Kanisheni ya Polisi Jamii Dk, Ezekiel Kyogo, amesema wameshiriki tamasha hilo kwa lengo la kutoa elimu Kwa jamii.
Amesema matukio mengi ya jinai chimbuko lake ni kukosekana maadili, hivyo kupitia elimu hiyo wataweza kurejesha jamii kwenye maadili.
Naye Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro, Pendo Meshurie amesema kupitia tamasha hilo wamekuwa wakitoa elimu ya kupambana na vitendo vya ukatili kupitia sanaa zikiwemo nyimbo na vipeperushi.



