Polisi Pwani yawabaini wanafunzi wasioripoti shuleni

PWANI: JESHI la Polisi Mkoani Pwani limemebaini baadhi ya wanafunzi walioshindwa kuripoti shuleni kunatokana na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na migogoro ya kifamilia.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Mjini Kibaha, Kamanda wa Polisi mkoani Pwani, Salim Morcase, amesema kuwa hayo yamebainika mwezi Julai kutokana na mpango kazi wa kufuatilia wanafunzi ambao hawajaripoti shuleni wakiwemo watoro sugu.
Mocase amesema kuwa katika kipindi hicho jumla ya wanafunzi 573 wa Shule za Msingi na Sekondari hawakuripoti Shuleni ambapo kati yao 114 wamerudishwa Shule.
Amesema kuwa changamoto nyingine ni mimba za utotoni ukosefu wa mahitaji ya msingi kama vile sare za Shule na madaftari na changamoto za kiafya na kiuchumi.
Kati ya hao wanafunzi ambao hawakuripoti wa Shule za Msingi walikuwa 251 na wa Sekondari walikuwa ni 322 ambapo wanafunzi hao walibainika katika kipindi hicho.
Amewataka wazazi na walezi kushirikina na viongozi wa dini na wa kiserikali katika kupambana na viashiria vya vitendo vya ukatili wanavyofanyiwa watoto ndani ya jamii.



