Samia: 2025 matumaini makubwa

Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.

RAIS Samia Suluhu Hassan amesema mwaka huu wa 2025 utakuwa wa mafanikio na matumaini yatakayoamua kesho bora ya nchi kutokana na mipango ya utekelezaji wa Falsafa ya R4 na mafanikio makubwa yaliyopatikana mwaka jana.

Rais Samia alisema hayo katika salamu zake za kukaribisha Mwaka Mpya wa 2025, ambazo alisema serikali itaendelea na mchakato wa kupata maoni ya wananchi ili kukamilisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ili utekelezaji uanze.

“Nilianza kwa kusema kuwa mwaka tunaoumaliza ulikuwa mwaka wa kihistoria, wenye mafanikio na unaotupa matumaini zaidi kuhusu kesho ya Taifa letu na maelezo yangu yameonesha kwa nini nilisema hivyo,” alisema.

Advertisement

“Nikihitimisha, niseme tu kwamba, mwenendo mzuri wa uchumi, uwezo wa kukabiliana na changamoto na kusimamia mipango yetu, na ari kubwa ya wananchi kujiletea maendeleo, vinatupa sote matumaini makubwa sana tunapoingia mwaka 2025,” alisema Rais Samia katika salamu zake.

Alibainisha kuwa mapema mwaka huu, serikali inatarajia Reli ya Kisasa (SGR) ianze kusafirisha mizigo kwa vipande vya Dar es Salaam hadi Dodoma tani milioni moja kwa mwaka, lengo ni kukuza ushoroba wa kibiashara na kimaendeleo unaochochea uzalishaji na ajira kwa wananchi kote inapopita.

Vilevile, Rais Samia alidokeza kuwa serikali itakamilisha kipande cha reli Mwanza hadi Isaka na kukifanya kianze kutoa huduma. Ujenzi wa vipande vingine hadi Kigoma vitaendelea kujengwa kama ilivyopangwa.

Alisema mwaka huu serikali inatarajia kupokea Ripoti ya Tume ya Rais ya Maboresho ya Kodi ambayo itasaidia kuboresha wigo na mifumo ya kodi, pamoja na kustawisha mazingira ya kibiashara nchini.

Alisema katika utekelezaji wa mapendezo ya Tume ya Hakijinai, serikali itakamilisha sera na kufanya marekebisho ya sheria mbalimbali zinazohusiana na masuala ya hakijinai.

Pia, alisema serikali itaendelea kutoa msaada wa kisheria kwa wahitaji ambao hadi sasa wananchi 495,552 wameshanufaika na msaada wa kisheria wa Kampeni ya Mama Samia chini ya Wizara ya Katiba na Sheria.

“Mwaka huu ni maalumu kwa maendeleo ya kisiasa na kidemokrasia nchini. Tutafanya Uchaguzi Mkuu kuwachagua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wabunge na madiwani, na kwa upande wa Zanzibar, tutachagua Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na madiwani,” alisema Rais Samia.

Aliongeza kuwa miongoni mwa maandalizi ya awali ya uchaguzi huo ni kufanya mashauriano na wadau wote wa kisiasa yaliyofanya kurekebishwa kwa Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani, Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, na Sheria ya Vyama vya Siasa.

“Ni imani yetu kwamba sheria hizo zitatuongoza vyema katika kusimamia kwa ufanisi chaguzi zijazo. Nitoe rai kwa wananchi na wadau wote wa uchaguzi kuhakikisha tunaidumisha sifa ya nchi yetu ya kuwa na demokrasia iliyojengeka juu ya msingi wa uhuru na haki,” aliongeza.

Aidha, Rais Samia alisema mwaka huu serikali itakamilisha miradi ya kimkakati ikiwamo Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere, Daraja la Kigongo/Busisi ambalo limefikia asilimia 94, linalotazamiwa kukamilika Februari mwaka huu.

Alisema serikali pia itatoa kipaumbele katika utekelezaji wa miradi ya kupunguza msongamano katika miji mikubwa kama vile Dar es Salaam, Arusha, Mwanza, Mbeya na Dodoma na kurahisisha usafiri na usafirishaji katika miji inayokua kwa kasi.

“Miongoni mwa miradi hii ni mradi wa Barabara za Mzunguko katika Jiji la Dodoma ambao umefikia asilimia 80, upanuzi wa Barabara ya Uyole-Ifisi-Songwe Airport jijini Mbeya ambao umefikia asilimia 20, na Awamu ya Tatu na Nne ya miundombinu ya barabara za mwendo kasi Dar es Salaam, huku tukianza huduma kwenye Awamu ya Pili kwa njia ya Mbagala iliyokwishakamilika,” alifafanua.

Rais Samia alieleza pia kuwa mwaka huu serikali itaendelea kuimarisha na kusambaza huduma za kijamii kama vile afya, elimu, maji na umeme, kuchochea maendeleo kupitia ujenzi wa miundombinu, kuwaongezea fursa vijana na wanawake katika biashara ndogo na za kati na kuimarisha ustahamilivu wa taifa.

Sambamba na hayo, miradi mingine inayotazamiwa kuanza utekelezaji mwaka huu ni ujenzi wa barabara ya haraka kutoka Kibaha – Chalinze kilometa 78.9, Mradi wa Ukaguzi wa lazima wa vyombo vya moto chini ya Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Polisi, Mradi wa Mabasi Yaendayo kwa Haraka (BRT) chini ya DART na Mradi wa Ujenzi wa Jengo la Biashara na Hoteli ya Nyota Nne katika Kiwanja cha Ndege cha Julius Nyerere (JNIA) chini ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA).

“Mwaka huu tutaendeleza mageuzi ndani ya serikali ili kuimarisha utendaji na ufanisi na utaratibu wa kubaini taasisi na mashirika yanayopaswa kufutwa, kuunganishwa au kurekebishwa kwa lengo la kuongeza tija na ufanisi zaidi,” alibainisha Rais Samia.

Alisisitiza kuwa serikali itaendelea kuchukua hatua za kuimarisha sekta ya ushirika ili kuchochea maendeleo vijijini na kwamba dhamira ya Serikali ni kurejesha hadhi ya ushirika nchini ili kupata maendeleo endelevu kwa ushirika na wanaushirika.

Vilevile alisema serikali itaendelea kushirikisha sekta binafsi na kuhamasisha uwekezaji kwa njia ya ubia baina ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP) ili kuongeza ufanisi katika sekta za uzalishaji na huduma.

Alisema katika kufanikisha hilo mpaka sasa kuna jumla ya miradi 74 ya ubia ambayo ipo katika hatua mbalimbali za maandalizi na utekelezaji.