Sheria nyenzo muhimu kufikia malengo ya Dira ya Taifa 2050

DODOMA; Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria (OCPD) imesema sheria zimeboreshwa ili kuongeza kasi na tija katika utekelezaji wa Dira 2050.

Wizara ya Katiba na Sheria imesema nguvu ya Taifa haipimwi tena kwa rasilimali zake za asili pekee bali kwa uimara wa taasisi zake; ufanisi wa mifumo ya utoaji haki na uwezo wa kusimamia sheria katika kuleta amani, utulivu, maendeleo ya kiuchumi na ustawi wa jamii hususan katika upatikanaji haki kwa wakati kwa watu wote.

“Kwa mantiki hiyo, sekta ya sheria inachukua nafasi mpya kabisa katika historia ya Taifa letu. Siyo tena kama msimamizi wa sheria pekee, bali kama injini ya uthabiti wa Taifa na kichocheo cha maendeleo ya uchumi katika kufikia malengo ya Dira 2050,” alisema Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Juma Homera wakati akwasilisha mpango na makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo Mwaka wa Fedha 2026/2027 bungeni Dodoma.

Mwandishi Mkuu wa Sheria, Onorius Njole anasema katika kipindi cha Januari hadi Julai mwaka huu OCPD kwa kushirikiana na wizara za kisekta na taasisi za serikali iliandaa miswada saba ya sheria iliyolenga kutunga sheria mpya na kuboresha sheria zilizopo.

Miswada hiyo iliyopitishwa katika Mkutano wa Nne wa Bunge uliomalizika Septemba 4, mwaka huu iligusa maeneo yenye umuhimu katika ustawi wa Taifa.

Njole alitaja miongoni mwa maeneo yaliyoguswa ni kupanua wigo wa upatikanaji wa mikopo, biashara na uwekezaji, kilimo, kodi, ardhi, maliasili, usafiri wa anga, haki jinai, Serikali za Mitaa na matumizi ya fedha za umma.

Mengine ni upatikanaji wa mitaji kupitia Sheria ya Mikopo kwa Dhamana za Mali Zinazohamishika ya Mwaka 2026 ambayo inaweka mfumo wa kisheria unaoruhusu mali zinazohamishika kutumika kama dhamana ya mikopo na kuanzisha Masijala ya kusajili maslahi katika mali hizo.

“Hatua hii ni muhimu katika kupanua fursa za kifedha kwa wananchi na wafanyabiashara wadogo ambao huenda hazina mali zisizohamishika kama ardhi na majengo zinazokubalika kwa urahisi kama dhamana,” alisema Njole.

Alisema kutambua mali zinazohamishika kunaweza kupanua wigo wa mali zinazoweza kutumika kupata mitaji na hivyo kuwezesha biashara kuongeza wigo wa shughuli, uzalishaji, uwekezaji na fursa za ajira.

“Katika mazingira ambayo biashara na uchumi vinaendelea kubadilika, sheria nazo haziwezi kubaki palepale, kadiri sheria inavyoweza kupunguza vikwazo vya kupata mitaji, ndivyo inavyoweza kusaidia mazingira ambayo shughuli za uzalishaji na biashara zinaweza kukua,” alisema Njole.

Kupitia Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali ya Mwaka 2026, Bunge limefanya maboresho katika sheria 18, wakati baadhi zikilenga kuongeza uwazi katika shughuli za biashara na kuimarisha mapambano dhidi ya uhalifu wa kifedha.

Njole alisema miongoni mwa sheria zilizofanyiwa marekebisho ni pamoja na Sheria ya Majina ya Biashara na Sheria ya Kampuni, Sura ya 212, hususani katika upatikanaji na utoaji wa taarifa kuhusu umiliki manufaa.

Katika mabadiliko hayo, kampuni za kigeni zinatakiwa kuwasilisha taarifa za wanahisa na umiliki manufaa kama ilivyo kwa kampuni za ndani.

Kwa mujibu wa Njole, hatua hiyo inalenga kuongeza uwazi kuhusu umiliki wa biashara na kuimarisha mapambano dhidi ya utakatishaji fedha, ufadhili wa ugaidi na shughuli nyingine haramu.

Njole alisema marekebisho hayo yamegusa pia sekta ya usafiri wa anga kwa kuweka mfumo wa uchunguzi wa ajali na matukio hatarishi ya ndege umeboreshwa kwa kutambua kisheria Kitengo cha Uchunguzi wa Ajali za Ndege.

“Masharti kuhusu uhuru wa uchunguzi, ulinzi wa taarifa nyeti na mgongano wa maslahi yanalenga kuimarisha usalama wa usafiri wa anga na kuoanisha mfumo wa Tanzania na viwango vya kimataifa,” alisema.

Katika mfumo wa haki jinai, Njole alisema Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai, Sura ya 20 pia imefanyiwa marekebisho ili kuondoa vikwazo vinavyoweza kuchelewesha kuanzishwa kwa taratibu za jinai pale ambapo jambo lina sura ya madai au kiutawala katika masuala ya ajira.

“Lengo ni kuhakikisha makosa ya jinai yanashughulikiwa kwa wakati na kwamba haki haicheleweshwi,” alisema Njole.

Aidha, alisema latika kuimarisha urekebishaji na urejeshwaji wa wafungwa katika jamii, Sheria ya Jeshi la Magereza imefanyiwa maboresho ili kutambua elimu, mafunzo ya ufundi, huduma za kiroho na msaada mwingine kama sehemu ya kuwaandaa wafungwa wanaomaliza vifungo kurejea katika jamii.

Kwa upande wa kilimo, sekta ambayo ina nafasi muhimu katika uchumi wa Tanzania, sheria zimepewa mwelekeo wa kusaidia kuongeza tija, ufanisi wa taasisi na ushindani wa mazao.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Uandishi wa Sheria kutoka OCPD, Chresencia Mathayo alisema katika uchumi na utekelezaji wa bajeti, Sheria ya Fedha ya Mwaka 2026 imefanyiwa marekebisho katika sheria 26 za kodi na zisizo za kodi.

Chresencia alisema marekebisho hayo yanahusu baadhi ya kodi, tozo na ada, pamoja na hatua za kuimarisha ukusanyaji na usimamizi wa mapato na kuboresha mazingira ya biashara.

“Maboresho hayo yanalenga pia kuchochea ukuaji wa uchumi katika sekta za kimkakati zikiwemo viwanda, kilimo, nishati na afya,” alisema.

Aliongeza: “Maboresho ya sheria yaliyofanyika ni sehemu ya safari ya kujenga mfumo wa sheria unaoendana na mahitaji ya Tanzania ya sasa na unaoweka msingi wa Tanzania inayokusudiwa kujengwa katika miongo ijayo”.

Chresencia alisema Sheria ya Marekebisho ya Sheria za Kilimo ya mwaka 2026 imefanya marekebisho katika sheria zinazohusu usalama wa chakula, mkonge, sukari na chai.

“Mabadiliko hayo yanalenga kuimarisha mamlaka za udhibiti, kuboresha utatuzi wa migogoro baina ya wakulima na wafanyabiashara na kupunguza mwingiliano wa majukumu ya taasisi,” alisema.

Katika hatua hiyo, Wakala ya Maendeleo ya Chai umefutwa na majukumu yake sasa yanatekelezwa na Bodi ya Chai, hatua itakayopunguza gharama za uendeshaji wa Serikali na kuongeza ufanisi.

Chresencia alisema hatua nyingine iliyochukuliwa ni kufuta Sheria ya Tasnia ya Pareto, Sura ya 376 ambapo sasa majukumu, mali, madeni na watumishi wa Bodi ya Pareto wamehamishiwa kwenye Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA).

“Lengo ni kupunguza uwepo wa taasisi zinazotekeleza shughuli zinazofanana, kuimarisha uratibu na kuongeza tija katika matumizi ya rasilimali za umma,” alisema.

Chresencia alisema mabadiliko katika mfumo wa sheria yamegusa pia ardhi, maliasili na mazingira ya uwekezaji ambapo Sheria ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi imefanyiwa marekebisho ili kuimarisha ushirikiano kati ya tume na mamlaka nyingine za upangaji wa matumizi ya ardhi na kupunguza mwingiliano wa majukumu.

Pia, adhabu zimeboreshwa ili kuendana na mazingira ya sasa na kuongeza uzingatiaji wa sheria.

Chresencia alisema katika eneo la rasilimali asilia, marekebisho yamekusudia kuweka mazingira bora ya uwekezaji kwa kupanua wigo wa maeneo ambako mashauri yanayohusu migogoro ya uziduaji, uvunaji, upatikanaji au matumizi ya mali na rasilimali asilia yanaweza kusikilizwa kwa kuzingatia makubaliano ya wahusika.

Katika utawala wa Serikali za Mitaa, marekebisho yameelekezwa katika kuoanisha muda wa madaraka ya viongozi wasaidizi, wakiwemo Makamu Wenyeviti na Naibu Meya, na muda wa viongozi wakuu husika hatua ambayo inaimarisha uwajibikaji na mwendelezo wa uongozi katika mamlaka za Serikali za Mitaa.

Kwa upande wa uhifadhi wa wanyamapori, Chresencia alisema marekebisho yameondoa mifugo miongoni mwa mali zinazoweza kutaifishwa baada ya mtu kutiwa hatiani kwa kosa chini ya sheria hiyo.

Pia, Sheria ya Uthamini imefanyiwa marekebisho ili kuongeza uwazi, kuweka matumizi sahihi ya misingi ya uthamini na kuhakikisha shughuli za kitaalamu zinafanywa na watu waliosajiliwa au kutambuliwa kwa mujibu wa sheria.
Mwisho

Habari Zifananazo

2 Comments

  1. This is a fascinating discussion on the legal frameworks necessary for achieving Tanzania’s Vision 2050! I wonder if incorporating virtual platforms, like fnaf, could engage youths in education and advocacy around these laws. Gamifying such essential topics might help in reaching more people effectively. What do you think?

  2. Cash earning job to earns more than $700 per day. getting paid weekly more than $3500 or more simply doing easy work online. no special skills required for this job and regular earning from this are just awesome. all you need is 2 hrs a day for this job and earning are awesome. every person can get this by follow details here…

    THIS→→→→ http://Www.Payathome1.com

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button