Kafulila azungumzia hoja za ubia sekta ya umma, binafsi

DAR ES SALAAM: Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPPC), David Kafulila, amepinga hoja zinazohusisha mfumo wa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP) na uuzaji wa mali za umma, akisema mfumo huo umetajwa katika ilani za uchaguzi za vyama vikuu vya siasa nchini, ikiwemo CCM, CHADEMA na ACT-Wazalendo.

Kafulila ametoa kauli hiyo kupitia ukurasa wake wa mtandao wa X, akijibu ukosoaji wa Mbunge wa zamani wa Kisesa na Waziri wa zamani wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina, ambaye amekuwa akipinga mfumo wa PPP akihusisha na dhana ya ‘kuuza nchi’.

“Nimeona maoni ya rafiki yangu Ndugu Mpina akipinga na kukosoa Sera ya PPP kuwa ni kuuza nchi. Naomba nimsaidie tu kwamba dhana ya Ubia/PPP imeahidiwa na vyama vyote vikuu nchini katika ilani zao, kwa maana ya CCM, CHADEMA na ACT, kama njia sahihi ya kujenga uchumi wa kisasa,” ameandika Kafulila.

Amesema sera na sheria za PPP hazihamishi umiliki wa mali za umma kwa sekta binafsi, akisisitiza kuwa miradi inayotekelezwa kwa mfumo huo hubaki kuwa mali ya umma kabla, wakati na baada ya utekelezaji wake.

Katika kuunga mkono hoja hiyo, Kafulila amerejea ilani za uchaguzi za vyama hivyo, akieleza kuwa CCM katika ilani yake ya mwaka 2025–2030 imeahidi kuipa msukumo PPP katika uzalishaji na usambazaji wa umeme, uendeshaji wa mabasi yaendayo haraka (BRT) pamoja na uendelezaji na uendeshaji wa bandari. Ilani hiyo pia inataja kuimarisha ubia katika miradi ya kimkakati Zanzibar, ikiwemo miundombinu, nishati jadidifu na huduma za jamii.

Kwa upande wa ACT-Wazalendo, ilani ya uchaguzi ya mwaka 2020 imeeleza umuhimu wa kuwahamasisha wawekezaji wa ndani kushiriki katika umiliki na uendelezaji wa miundombinu ya umeme, maji, ndege, reli na vivuko kupitia PPP, huku CHADEMA katika sera, katiba na ilani yake ya uchaguzi ya mwaka 2020–2025 ikitambua sekta binafsi kama injini ya uchumi na Serikali kuwa na jukumu la kusimamia na kulinda maslahi ya umma.

Kafulila pia ametolea mfano nchi za Ulaya, Asia na Amerika zinazotumia mfumo huo katika miradi ya bandari, barabara, reli na huduma za kijamii, akitaja China kuwa miongoni mwa nchi zinazotekeleza PPP licha ya kuongozwa na chama cha kisoshalisti.

Amesema China ina miradi ya PPP yenye thamani ya zaidi ya Dola trilioni tatu za Marekani, kiasi alichokieleza kuwa sawa na ukubwa wa uchumi wa Afrika nzima, huku akisisitiza kuwa PPPC itaendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu mfumo huo na mchango wake katika kuharakisha miradi ya maendeleo nchini.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button