Serikali yaombwa kugharamia matibabu ya vitiligo

DAR ES SALAAM: MWANZILISHI wa Taasisi ya Beyond Skin Initiative, Clementina Chalamila, ameiomba Serikali kuweka utaratibu wa kutoa matibabu ya vitiligo bila malipo, ambapo amesema huduma hiyo inapaswa kupewa kipaumbele kama ilivyo kwa dawa za kufubaza virusi vya UKIMWI (ARVs), ili kuwasaidia watu wengi wanaoshindwa kumudu gharama za matibabu.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na Daily News Digital, Chalamila amesema watu wengi wanaoishi na vitiligo hukabiliwa na changamoto za kifedha zinazowazuia kupata matibabu, huku wengine wakikata tamaa kutokana na gharama kubwa pamoja na unyanyapaa unaoendelea katika jamii.
Amesema hali hiyo imewafanya baadhi ya watu kushindwa kushiriki kikamilifu katika shughuli za kijamii na kiuchumi, huku wengine wakikosa ujasiri wa kuwania nafasi mbalimbali kwa hofu ya kuhukumiwa kutokana na mwonekano wa ngozi yao.
Chalamila amesema uzoefu wake binafsi unaonyesha kuwa vitiligo haiathiri uwezo wa mtu kufanikiwa, bali changamoto kubwa ipo katika mtazamo wa jamii, ambapo ameeleza kuwa baada ya kujikubali, aliamua kuanzisha Beyond Skin Initiative ili kutumia uzoefu wake kuwapa matumaini, elimu na hamasa watu wengine wanaoishi na hali hiyo.
Ameeleza kuwa iwapo Serikali itaweka utaratibu wa kutoa matibabu ya vitiligo bila malipo, watu wengi zaidi watajitokeza kutafuta huduma za afya badala ya kuendelea kujificha kwa sababu ya gharama kubwa za matibabu na hofu ya unyanyapaa.
Aidha, amesema hatua hiyo itachangia kuongeza uelewa wa jamii kuhusu vitiligo, kupunguza ubaguzi na kuwapa matumaini watu wanaoishi na hali hiyo ili waendelee kutimiza malengo yao bila vikwazo vinavyotokana na mitazamo hasi.



