Sh bilioni 1.2 kujenga kituo cha kutunza wazee Kigoma

TAASISI isiyo ya kiserikali ya Endeleza Wazee Kigoma (EWAKI) inatarajia kutumia kiasi cha Sh bilioni 1.2  kwa ajili ya ujenzi wa majengo manane yatakayotumika kutoa huduma ya makazi na malazi ya wazee mkoani Kigoma.

Mkurugenzi mtendaji wa taasisi hiyo, Cotilda Kokupima alisema hayo katika hafla ya harambee ya ujenzi wa kituo cha kuhifadhia na kusaidia wazee kwenye kata ya Nyumbigwa wilayani Kasulu mkoani humo.

Kokupima alisema kuwa ujenzi wa kituo hicho ni matokeo ya ushuhuda  wa mateso na manyanyaso wanayoyapata wazee ambayo yanayofanya wengi wao kuishi maisha yasiyo na furaha, kuishi mtaani bila matunzo hivyo ujenzi wa kituo hicho unalenga kuwapatia matunzo na mahitaji muhimu wazee ambao wametelekezwa na hawana mahali pa kupata mahitaji yao.

Advertisement

Mkurugenzi huyo alisema kuwa katika kituo hicho wanatarajia kujenga majengo manane ambayo yatakuwa na jengo la kliniki, ofisi za watendaji, jengo la kufanyia mazoezi mbalimbali, kumbi za mikutano na majengo kwa ajili ya mahitaji mengine muhimu kwa jumuia ya wazee na watendaji watakaokuwa maeneo hayo.

Mmoja wa wazee waliohudhuria hafla hiyo, Gerlad Nkona (65) mtumishi mstaafu wa serikali alisema kuwa wazee wengi wamekuwa kwenye matatizo makubwa kutokana na maisha wanayoishi sasa hata kama wakati wa ujana wao walikuwa na maisha mazuri.

Nkona alisema kuwa wapo wazee wametelekezwa na watoto wao na familia zao na sasa wanaishi mtaani wakiwa hawawezi kupata mahitaji yao muhimu ikiwemo chakula na mavazi hivyo kuishia kuwa omba omba hata kama wengine watoto wao ni watumishi wa serikali au taasisi wakiwa na uwezo mkubwa kifedha.

Naye Mzee Abdallah Ndayeza alisema kuwa licha ya wazee wengi kutelekezwa na kukosa matunzo lakini pia wamekuwa hawapati msaada hata wa kiserkakli hasa kwenye matibabu na wazee wengi ambao hawana uwezo kiuchumi wamekuwa wakihangaika namna ya kupata matibabu.

Hata hivyo alisema kuwa mahusiano mabaya baina ya wazee na watoto wao ni moja ya mambo yanayofanywa wazee kutelekezwa na kwamba kwa wale wenye matatizo ya kupata malazi na  misaada mingine ujenzi wa kituo hicho utakuwa faraja kubwa kwao.

Akizungumza katika hafla hiyo Mkuu wa wilaya Kasulu,Kanali Isack Mwakisu alisema kuwa kuanzishwa kwa mpango huo wa kuhifadhi wazee kunakofanywa na taasisi ya EWAKI kunatokana na juhudi kubwa ya serikali ikiwemo upatikanaji wa eneo husika na misaada mbalimbali ikiwemo ya kifedha kwa taasisi hiyo.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *