Simba: Tunataka ushindi Angola

DAR ES SALAAM; KOCHA Mkuu wa Simba, Fadlu Davids amesema anaenda Angola kutafuta ushindi kwenye mchezo wa raundi ya tano wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Maquis do Bravos, Uwanja wa Nacional Da Tundavala, Jumapili.
Simba inahitaji sare kwenye mchezo huo ambayo itaifanya kufikisha pointi 10 ambazo zitaweza kufikiwa na CS Constantine na hivyo kufuzu robo fainali ya mashindano hayo.
Bravos inashika nafasi ya tatu ikiwa na pointi sita huku CS Sfaxien ya Tunisia ikishika mkia bila pointi.
Akizungumza Dar es Salaam jana akitokea Tunisia ambako walipata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya CS Sfaxien, Fadlu alisema mechi yao dhidi ya Bravos ni muhimu kwani ndio itakayowavusha kwenda robo fainali.
“Utakuwa mchezo mgumu kwa sababu wapinzani wetu wakiwa kwao walishinda dhidi ya CS Constantine na CS Sfaxien, hivyo licha ya kuwa tunahitaji sare kufuzu, sisi tutafanya jitihada zote kushinda mchezo huu,” alisema Fadlu.
Kwa upande wake, Meneja Habari na Mawasiliano wa timu hiyo, Ahmed Ally alisema maandalizi ya safari yatakamilika na wataondoka kesho kuelekea Angola.



