SKA 2026: Upigaji Kura Waanza Leo

ZOEZI la upigaji kura kwa wananchi katika Tuzo za Uandishi wa Habari na Makala za Maendeleo yaani Samia Kalamu Awards (SKA) 2026 linaanza leo, Septemba 3, na litaendelea hadi Septemba 30, mwaka huu.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa zoezi la upigaji kura Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Peter Mwasalyanda, amesema wananchi wanaweza kushiriki kupiga kura kupitia tovuti ya www.samiaawards.tz au kwa kutumia ujumbe mfupi wa simu (SMS), kwa kutuma neno AKA likifuatiwa na namba ya mshiriki na kutuma kwenda namba 15200.

Hatua hiyo imefikiwa baada ya kazi 294 kufuzu kwa ajili ya kupigiwa kura na wananchi zilizowasilishwa katika awamu ya pili ya tuzo hizo. Mwasalyanda ameshukuru waandishi wa habari kwa mwitikio mkubwa waliouonesha kwa kuwasilisha kazi zao ambazo zilikuwa 3003. “Tuzo za Samia Kalamu Awards zimeendelea kusaidia kuhamasisha waandishi wa habari kushindanisha kazi zao ili ziweze kuingia katika tuzo hizo”, amesema Mwasalyanda.

Kwa mwaka jana jumla ya wananchi 60,638 walishiriki kupiga kura, huku akieleza kuwa mwaka huu wanatarajia idadi hiyo kuongezeka zaidi. Amesema wananchi wote wataweza kushiriki kupiga kura hata kama wapo vijijini, kwa kuwa tuzo hizo zimezingatia ushiriki kuanzia ngazi ya taifa hadi ngazi ya chini. SOMA: Tuzo za Samia kalamu awards kutolewa Mei

Miongoni mwa makundi yaliyopo katika tuzo hizo ni pamoja na Redio za Jamii Vijijini, hatua inayowazingatia watu wa vijijini ili waweze kupiga kura kiurahisi zaidi. Mwasalyanda ametoa wito kwa wadau mbalimbali, zikiwamo taasisi, kampuni na mashirika, kuendelea kujitokeza na kudhamini Samia Kalamu Awards 2026, akisema hatua hiyo itasaidia kuhamasisha uandishi wa habari wenye ubora, weledi na uwajibika.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button