Tamisemi yaboresha tovuti kuongeza ufanisi taarifa kwa wananchi

OFISI ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), imeanza uboreshaji wa tovuti zake ili kuendana
na mabadiliko ya teknolojia na kuongeza ufanisi wa utoaji wa taarifa kwa wananchi.

Uboreshaji huo unatekelezwa kwa kushirikiana na Mradi wa Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) wa Uimarishaji wa Mifumo ya Sekta za Umma Awamu ya Pili (USAID PS3+).

Akizungumza mkoani Morogoro, Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano Serikalini, Ntenghenjwa
Hosseah alisema lengo la uboreshaji ni kurahisisha uendeshaji wa tovuti hizo, hususani tovuti za Tamisemi,
sekretarieti za mikoa na mamlaka za serikali za mitaa kupitia mfumo wa tovuti wa serikali (Government Website Framework-GWF).

SOMA: Wadau wa uchaguzi waikingia kifua TAMISEMI

Hosseah alifafanua maboresho hayo yanaendana na mkakati wa kidijiti wa serikali unaolenga kurahisisha matumizi ya teknolojia kwa wananchi pamoja na kuhakikisha tovuti hizo zinatoa maudhui bora na sahihi kwa
urahisi.

Alisema mabadiliko hayo yanalenga kuboresha mwonekano, maudhui, kurahisisha upatikanaji na ufikiaji
wa tovuti hizo kwa urahisi na yataleta mabadiliko makubwa katika utoaji wa habari zauhakika kwa wananchi.

Pia alisema maboresho ya mfumo wa GWF yatasaidia tovuti za Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za
Serikali za Mitaa kuwa jukwaa la kutoa habari zilizo sahihi zenye maudhui rahisi na kufikika kwa urahisi kulingana na kasi ya ukuaji wa teknolojia kwa kukabiliana na teknolojia mpya na mahitaji ya udhibiti kwa urahisi.

SOMA: Bajeti Tamisemi yapita

Mkurugenzi wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) wa Tamisemi, Erick Kitali alisema maboresho
hayo ni sehemu ya utekelezaji wa Mkakati wa Uchumi wa Kidijiti Tanzania (2024-2034) na yanalenga kuboresha
usalama wa tovuti, kuongeza uwazi na kurahisisha upatikanaji wa huduma na taarifa za serikali kwa wananchi.

Habari Zifananazo

Back to top button