Tume ya Madini yatoa hati za makosa kwa miradi 42

DODOMA: Tume ya Madini imewaonya wamiliki wa miradi ya uchimbaji mdogo wa madini yenye Mikataba ya Msaada wa Kiufundi (TSA) kuwa itachukua hatua za kisheria, ikiwemo kufuta ridhaa za Msaada wa Kiufundi, iwapo watashindwa kurekebisha mapungufu yaliyobainika ndani ya siku 30.
Onyo hilo limekuja baada ya tume hiyo kukagua jumla ya miradi 128, ambapo miradi 42 ilibainika kuwa haifanyi kazi na kupewa Hati za Makosa za siku 30, huku miradi 86 inayofanya kazi lakini ikiwa na mapungufu ikiagizwa kuyarekebisha ndani ya muda huo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Agosti 26, 2026, Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Ramadhan Lwamo, amesema ukaguzi huo umefanyika kufuatia maelekezo ya Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, aliyoyatoa Aprili 27, 2026 wakati akiwasilisha bajeti ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/2027.
Amesema miradi 86 inayofanya kazi imebainika kuwa na changamoto katika kutekeleza masharti ya Mikataba ya Msaada wa Kiufundi pamoja na matakwa ya Sheria ya Madini, Sura ya 123.
“Kwa miradi 42 iliyobainika kuwa haifanyi kazi, Hati za Makosa za siku 30 zimetolewa kwa wamiliki husika na kama hakutakuwa na mrejesho chanya ndani ya muda uliotolewa, taratibu za kisheria zitafuata, ikiwemo kufuta ridhaa ya utoaji wa Msaada wa Kiufundi,” amesema Lwamo.
Kwa mujibu wa Tume, baadhi ya miradi inayofanya kazi imeshindwa kutekeleza ipasavyo mipango inayotakiwa kisheria, ikiwemo Mpango wa Usimamizi wa Mazingira, Mpango wa Uwajibikaji kwa Jamii (CSR), Mpango wa Uhawilishaji wa Teknolojia, Mpango wa Uchimbaji na Mpango wa Ufunguaji wa Mgodi.
“Wamiliki na wawezeshaji wa Msaada wa Kiufundi wameelekezwa kurekebisha mapungufu yao kwa mujibu wa Kanuni za Msaada wa Kiufundi kwa Wamiliki wa Leseni Ndogo za Uchimbaji Madini za Mwaka 2025, ndani ya siku 30,” amesema.
Aidha, Tume imesema itaendelea kufanya ukaguzi wa mara kwa mara katika miradi hiyo ili kuhakikisha inatekelezwa kwa mujibu wa sheria, kanuni na masharti ya ridhaa zilizotolewa.
Tume pia imewataka wachimbaji wadogo kuzingatia utunzaji wa mazingira, usalama na afya kazini, huku ikisisitiza kuwa Msaada wa Kiufundi umewekwa kisheria ili kuwawezesha wachimbaji wadogo wasiokuwa na uwezo kuendeleza maeneo yao, kuongeza tija na uzalishaji pamoja na kupata teknolojia bora za uchimbaji na uchenjuaji wa madini.




Simple, fast, and effective. I don’t like overcomplicated sites and this one gets straight to the point. I really like aa444 for its efficiency.