“TUNATAKA kila mtu hapa Tanzania azijue haki za watoto. Children Support Tanzania kupitia Noela na watu wengine Tanzania wanafanya kazi nzuri. Tutashuhudia kutiwa saini kwa mkataba ili Noela aweze yale anayopaswa kuyafanya hasa katika haki za watoto na kila mtoto Tanzania aende shule hasa mwenye ulemavu.”
Ni maneno ya faraja kwa jamii ya watoto wanaokabiliwa na changamoto ya ulemavu wa aina mbalimbali ikiwemo wa viungo na wenye utindio wa ubongo.
Balozi wa Ujerumani nchini, Regine Hess ndiye aliyetamka maneno haya alipotembelea shule jumuishi ya msingi iliyopo chini ya kituo cha kulelea watoto walio na ulemavu cha Child Support Tanzania (CST) cha jijini Mbeya.
Kituo hicho ni sehemu ya wanufaika wa msaada wa Sh bilioni moja zilizotolewa na Serikali ya Ujerumani kwa ajili ya uendeshaji wa shughuli mbalimbali nchini kupitia Shirika la Christian Blind Mission (CBM).
Tafiti zinaonesha kuwepo kwa watoto walio na ulemavu wanaonyimwa haki zao za msingi kutokana na wazazi au walezi kuona ulemavu wao ni kama laana kwa familia zao. Wengine hudhani kuzaliwa kwa watoto walemavu ni matokeo ya mizimu kuchukizwa na wazazi au jamii husika.
Kwa fikra hizo potofu watoto hawa wanabaguliwa, wanafungiwa ndani, wananyimwa chakula, hawapelekwi shule hata wanapofikia umri unaotakiwa waanze shule na kukosa uchangamshi wa pamoja na kuwafanya wajione wanyonge tangu wangali wadogo.
Nchini ipo Programu ya kitaifa inayoendelea kutekelezwa iitwayo PJT-MMMAM inayolenga kuleta uchechemuzi ndani ya jamii katika malezi ya msingi ya watoto kupitia vipengele vya afya bora, lishe kamili, ulinzi na usalama, malezi yenye mwitikio na ujifunzaji na uchangamshaji wa awali wa mtoto katika umri wa tangu miaka sifuri hadi minane. Watoto walio na umri huo walio na ulemavu pia inawahusu.
Kimsingi PJT-MMMAM imeyalenga zaidi maisha ya mtoto aliye na umri wa kuanzia miaka sifuri hadi atakapofikisha miaka minane. Ni kipindi kinachotajwa kuwa muhimu katika makuzi sahihi ya mtoto kwa kuwa ndicho kipindi pia muhimu katika ukuaji wa ubongo wake. Tafiti zinaonesha ukuaji wa ubongo wa mtoto katika kipindi hiki ni zaidi ya asilimia 90.
Wataalamu wa Elimu ya Sayansi ya Maendeleo ya Awali ya Mtoto (ECD) wanaeleza kuwa matokeo chanya ya malezi stahiki kwa kipindi hiki ndiyo yenye kufanya jamii kuwa na watu wenye utimilifu ukubwani na kuiwezesha kuwa na maisha stahiki.
Kutowekeza kikamilifu kwenye malezi ya awali ya mtoto ndiko kunasababisha jamii kuwa na watoto, vijana na watu wazima walio na changamoto nyingi ikiwemo msongo wa mawazo wa kudumu.
Walemavu waliotengwa na kunyimwa haki zao za msingi tangu wangali wachanga wanaweza kuishi na msongo wa mawazo wa kudumu hata watakapokuwa watu wazima.
Utekelezaji wa PJT-MMMAM unazipa pia nguvu Sera ya Mtoto ya Mwaka 2008 na Sheria ya Mtoto Namba 21 ya mwaka 2019 na Sheria ya Elimu ya Mwaka 1978 na marekebisho yake ya mwaka 2016. Hizi zote ni nyenzo za kuwezesha wadau wote kumjengea mtoto mazingira sahihi ya ukuaji wakiwemo watoto walio na ulemavu.
Balozi Regine anasema kinachofanywa na CST ni kazi nzuri lakini ili kituo hicho na vingine viweze kufanya yale yanayowezekana kila mmoja lazima azijue haki za watoto na kuhakikisha kila mtoto wa Tanzania anazipata ikiwemo mtoto aliye na ulemavu.
“Sisi Serikali ya Ujerumani tunataka kuona watoto wengi wanakwenda shule na waweze kupata huduma nzuri ya elimu, mazoezi na afya bora. Waimbe pamoja, wacheze pamoja kama ule wimbo wa kichwa, mabega na miguu mnaoimba siku zote,” anasema Balozi Regine.
Noela Shawa ndiye Mkurugenzi Mtendaji wa CST, anasema kumekuwepo na mwendelezo wa matokeo chanya ya mwamko wa wadau na wazazi walio na watoto walemavu kuanza kuwapeleka shule tofauti na ilivyokuwa awali. Sasa walemavu wanaoandikishwa shuleni hapo wanao umri mdogo sawa na watoto wasio na ulemavu yaani wengi ni walio na umri usiozidi miaka mitano.
“Wakati tunaanzisha kituo na shule hii ilikuwa vigumu kwa wazazi kutuelewa. Wengi kwa dhana potofu waliwafungia majumbani watoto waliopaswa kuanza shule. Kwa sasa mwamko upo na wengi wanafika kuuliza umri wa watoto wao iwapo tunaweza kuwapokea,” anasema Noela.
Mkurugenzi Mkazi wa CBM nchini, Nesia Mahenge alikitaja kituo cha CST kuwa cha mfano unaopaswa kuiga kwa kuwa na shule inayojumuisha watoto wa aina zote na kuwafanya wapate huduma ya ujifunzaji kwa pamoja pasipo kuwabagua walemavu.
Anawasihi wafanyakazi wa kituo hicho, wakazi wa maeneo ya jirani na wazazi wa wanafunzi kuendelea kuwa mabalozi kwa kuelezea kinachofanywa na kituo hicho ili kuwezesha wadau na wazazi wengine kuwabaini watoto walio na ulemavu waliofichwa majumbani ili wapelekwe shule.
Akimwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Elimu Maalumu nchini, Dk Magreth Matonya, Ofisa Elimu Maalumu wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya, Wende Mbilinyi alisema kituo hicho kimekuwa na msaada mkubwa katika utoaji elimu kwa watoto walio na ulemavu na yapo mafanikio makubwa yaliyopatikana tangu kuanzishwa kwake.
Mmoja wa wazazi wa watoto walio na ulemavu wanaosoma shuleni hapo, Joseph Paul aliitaja CST kuwa mkombozi wa maisha ya watoto wao kwa kuwa imeonesha njia sahihi ya kuwezesha watoto hao kufikia ndoto zao maishani mwao.
Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) linasema ujumuishwaji watoto wenye ulemavu si anasa bali ni haki. Ripoti iliyozinduliwa Novemba 10, 2021 jijini New York nchini Marekani lilibainisha kuwa idadi ya watoto wenye ulemavu duniani inakadiriwa kuwa takribani milioni 240.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo watoto wenye ulemavu wanakosa fursa ikilinganishwa na watoto wasio na ulemavu katika hatua nyingi za ustawi wa watoto, imesema ripoti hiyo mathalani mtoto 1 kati ya 10 anakosa mahitaji ya msingi ikiwemo afya, elimu na ulinzi.
Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF, Henrietta Fore kupitia ripoti hiyo anasema: “Utafiti huu mpya unathibitisha kile ambacho tayari tunakifahamu kuwa watoto wenye ulemavu wanakabiliwa na changamoto kubwa na mara nyingi athari limbikizi katika kutekeleza haki zao.”
Ripoti hiyo ilijumuisha takwimu kutoka nchi 42 na inashughulikia zaidi ya viashiria 60 vya ustawi wa watoto.
Kupitia makala haya ni muhimu jamii ikajitathmini kuona ni kwa jinsi gani mtoto mwenye ulemavu anajengewa uwezo wa kuja kuwa mtu mwenye mchango kwenye maendeleo atakapofikia ukubwani. Mazingira wezeshi ajengewe katika umri unaotajwa na PJT-MMMAM ili kutomfanya mpweke ukubwani.