Utalii wa maombi waibua fursa kiuchumi

ARUSHA: UTALII wa maombi umeendelea kuibua fursa mpya za kiuchumi na kuvutia wageni katika Ziwa Duluti, wilayani Arumeru, huku serikali ikiwataka wawekezaji kuongeza huduma na miundombinu ili kutumia kikamilifu uwezo wa eneo hilo katika kukuza utalii.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Hamad Hassan Chande, wakati wa ziara ya wajumbe wa kamati ya wizara hiyo waliotembelea Ziwa Duluti na kujionea shughuli mbalimbali za utalii, ikiwemo matumizi ya mitumbwi yenye makasia kwa matembezi ya ziwani pamoja na uwekezaji wa nyumba za kulala wageni na huduma nyingine zinazotolewa pembezoni mwa ziwa hilo.

Amesema Ziwa Duluti ni miongoni mwa maeneo yenye fursa kubwa za utalii kutokana na uwepo wa mazingira ya asili pamoja na shughuli za kiimani zinazowavutia wageni wanaofika kwa ajili ya maombi na ibada huku akisisitiza utalii wa kidini ni eneo lenye uwezo mkubwa wa kuongeza mapato na ajira kwa wananchi kwa kuwa imani ni jambo endelevu linalowafanya waumini kusafiri mara kwa mara.

“Wawekezaji wa ndani na nje ya nchi njema kuwekeza zaidi katika huduma za malazi, burudani na miundombinu mingine ya utalii ikiwemo uvuvi,shughuli hizo zinaweza kuongeza mvuto wa eneo endapo zitaendelezwa kwa kuzingatia kanuni za uhifadhi na mazingira, mchanganyiko wa utalii wa maombi, utalii wa ziwani na shughuli za kiuchumi unaweza kuongeza fursa kwa wananchi wanaozunguka,”

Huku Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Msitu wa Asili wa Ziwa Duluti, Peter Myonga, akisema eneo hilo lina upekee wa kuunganisha uhifadhi wa mazingira na shughuli za kiimani, jambo lililochochea kukua kwa utalii wa maombi.

Amesema wageni wanaofika kwa ajili ya maombi wameendelea kutumia eneo hilo huku Serikali kwa kushirikiana na jamii ikiweka mazingira ya kufanya shughuli hizo bila kuathiri uhifadhi wa msitu.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Timotheo Mnzava, amesema ziara ya kamati hiyo Ziwa Duluti imeonesha namna uwekezaji wa sekta binafsi unavyoweza kuchochea maendeleo ya utalii, akiwataka wawekezaji kuongeza huduma zinazoweza kuwafanya wageni kukaa muda mrefu katika eneo hilo.

Mnzava amesema uwepo wa mitumbwi na makasia unaongeza ladha ya utalii wa ziwani, huku wageni wakipata fursa ya kufanya matembezi juu ya maji na kujionea mandhari ya Ziwa Duluti, kwani shughuli hizo, zikiunganishwa na huduma za malazi na burudani, zinaweza kulifanya eneo hilo kuwa kivutio kikubwa zaidi kwa watalii.

.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button