CHAMA cha Wachimbaji Wadogo wa Madini wilayani Kahama mkoani Shinyanga (SHIREMA) kimepata viongozi wapya ambao wameahidi kusimamia suala la vijana wanaovamia kwenye migodi na makusanyo ya mapato ya serikali.
Viongozi hao walichaguliwa Septemba 21 na wajumbe 91 waliohudhuria mkutano maalum nakuchagua nafasi 15 ikiwa usimamizi ulifanywa na ofisa madini mkazi wa Mkoa wa Kimadini Kahama, Winfrida Mrema nakufunguliwa na Mkuu wa Wlaya, Mboni Mhita.
Baada ya kuchaguliwa kuwa mwenyekiti mpya Philipo Masse kwa kupata kura 48 nakumshinda mpinzani wake Amos Mbaga aliyepata kura 46 amesema wachibaji wadogo wasiibe washiriki kutoa mapato ya serikali na kuishauri wapatiwe maeneo wachimbe ili wajinyanyue kiuchumi.
“Nitaondoa wachimbaji wadogo kuonewa wanapopata eneo tayari mwekezaji anapatikana siku hiyo hiyo pia nitawashirikisha viongozi wenzangu kuhamasisha serikali kutoa elimu zaidi ya kutotumia Zebaki katika uchenjuaji madin,” amesemaMasse.
Ofisa Habari, Siasa, Mawasiliano na Jamii Steve Maige amesema wengi wanaamini wachimbaji hawana elimu kumbe sio kweli hawafikiwi vizuri na elimu watajitahidi na viongozi wenzake kuishauri serikali kuhakika wanaipata elimu na kuachana na utumiaji wa zebaki.
Mwenyekiti wa Shirema Mkoa wa Shinyanga Hamza Tandiko amesema viongozi hao wataongoza kwa kipindi cha miaka mitano huku akieleza atakaye kwenda kinyume cha kanuni,sheria na maadili wataomba kibali kutoka serikali ili kumuondoa.
“Viongozi tunaowataka wasiwe na uharakati wawe na ujuzi na wasio wajuaji nakuhakikisha madini hayatoloshwi nakuwa na mipango thabiti ya kuisaidia serikali sio kutengeneza migogoro,”amesema Tandiko.
Mkuu wa Wilaya ya Kahama Mboni Mhita amesema sekta ya madini imekuwa ni muhimu katika eneo la kukuza uchumi na sasa hakuna migogoro kwa wachimbaji wadogo sababu ushirikiano na serikali umekuwa ukienda na kuboreshwa zaidi ikiwemo kupatiwa leseni.