Wakulima Babati wanufaika programu ya AFDP

MANYARA: Wakulima wa vijiji vya Endasiko na Orng’adida, vilivyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Babati, mkoani Manyara, wameeleza kunufaika na Programu ya Kuendeleza Kilimo na Uvuvi (AFDP), inayofadhiliwa na Shirika la Kimataifa la Maendeleo ya Kilimo (IFAD) kwa kushirikiana na Serikali na kuratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu – Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu.

Wakulima hao walieleza hayo Septemba 4, 2026, wakati wa ziara ya timu kutoka IFAD iliyofanya tathmini ya maendeleo ya utekelezaji wa programu hiyo kupitia Tathmini ya Kipindi cha Kati (MTR).

Wakulima hao walisema programu hiyo imewawezesha kupata teknolojia za kisasa za kilimo mseto, ikiwemo matumizi ya mbegu himilivu zinazoweza kustahimili athari za mabadiliko ya tabianchi.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Bw. Ramadhani Iddi Mfumbilo, mkulima kutoka Kijiji cha Mkombozi, Kata ya Endasiko, alisema kupitia programu hiyo wakulima wamepata mbegu za mahindi aina ya Situka pamoja na mbegu za mazao ya lishe ambazo zimepandwa mashambani sambamba na mazao mengine, ikiwemo labulabu, yanayosaidia kurutubisha ardhi na kuzuia mmomonyoko wa udongo.

“Majani hayo pia si rafiki kwa mifugo kama vile ng’ombe. Hivyo, mifugo inapovamia shamba la mkulima, si rahisi kula au kuharibu mazao. Pia, yanasaidia kuwafukuza wadudu waharibifu wa mazao,” alisema.

Alibainisha kuwa mbegu za mazao ya lishe zina uwezo mkubwa wa kuboresha afya ya familia, hasa kwa watoto, kina mama wajawazito, wazazi na wazee, huku zikisaidia kupunguza tatizo la utapiamlo kwa watoto.

Aidha, akizungumzia mbegu za jamii ya mikunde, hususan maharage aina ya Jesca, alisema mbegu hizo zina virutubisho muhimu vinavyosaidia katika kuboresha afya, hasa kwa watoto.

Kwa upande wake, Bi. Naseriani Joseph, mkulima kutoka Kijiji cha Orng’adida, Kata ya Qash, alisema kupitia Programu ya AFDP wakulima wamepata elimu na mbegu bora za mazao ya lishe wanayolima katika bustani za nyumbani maarufu kama kitchen gardens.

Alisema kilimo hicho kimewanufaisha kwa kuwapatia mboga za kutosha majumbani, kuwasaidia katika mahitaji ya watoto shuleni na familia kwa ujumla, pamoja na kuimarisha afya na kuongeza kipato.

“Wanawake tunapata mahitaji yetu muhimu kupitia kilimo hiki, hususan mboga mboga na mazao ya mikunde. Tumepata elimu kuhusu maharage ya lishe, tumepata mbegu na tumezitumia. Maharage hayo yameboreshwa na yana virutubisho pamoja na madini ya chuma, hivyo afya za familia zinaimarika. Natoa wito kwa Serikali kuongeza upatikanaji wa mbegu hizi kwa kuwa ni adimu na zinazalishwa kwa uchache katika kata yetu,” alisema.

Wataalamu hao wanaendelea na ziara hiyo katika maeneo mbalimbali nchini yanayotekeleza programu hiyo katika sekta za kilimo na uvuvi, kwa lengo la kutathmini maendeleo ya utekelezaji wake.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button