Walimu Kilimanjaro walivyopewa mafunzo teknolojia Akili Unde

KILIMANJARO; Wakati Unde (AI) na teknolojia nyingine za kidijitali zikizidi kuwa sehemu ya maisha ya wanafunzi, walimu 215 wa shule za sekondari mkoani Kilimanjaro, wameanza mafunzo yanayolenga kuwabadilisha kutoka kuwa walimu wanaowasilisha taarifa pekee, hadi wawezeshaji wanaoweza kusaidia wanafunzi kuchambua, kuthibitisha na kutumia maarifa wanayoyapata kupitia teknolojia.
Mafunzo hayo ya wiki moja yamefanyika Chuo Kikuu Kishiriki cha Stefano Moshi Memorial (SMMUCo), Manispaa ya Moshi, yakiwa yameandaliwa na SMMUCo kwa kushirikiana na Teaching and Learning Advisory Group (TALAG), yenye makao yake nchini Uswisi.
Mafunzo hayo yanaibua mjadala mpana kuhusu nafasi ya mwalimu katika zama ambazo mwanafunzi anaweza kupata taarifa, mifano ya masomo na hata majibu ya maswali kupitia simu na intaneti kabla hajafika darasani.
Programu hiyo inafadhiliwa kwa pamoja na SMMUCo, Taasisi ya Bachschuster ya Uswisi, Globe Trotte Group, Taasisi ya Walo Kamm, Manispaa ya Hünenberg nchini Uswisi, pamoja na wafadhili wengine.

Kwa waandaaji wa mafunzo hayo, changamoto si kuwafanya walimu washindane na AI au teknolojia, bali kuwapa uwezo wa kuzitumia kama nyenzo za kuboresha ufundishaji.
Programu ya “Teaching and Learning with Digital Resources” inaeleza kuwa matumizi ya rasilimali za kidijitali yanapaswa kwenda sambamba na ufundishaji unaozingatia umahiri na mahitaji ya elimu ya wakati huu.
Teknolojia inamlazimisha mwalimu kubadilika
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, mwezeshaji mkuu, Prof Karl Fleischmann, alisema mabadiliko ya teknolojia yanawalazimu walimu kuendelea kujifunza ili wasibaki nyuma katika taaluma yao.
Alisema mafunzo hayo hayalengi kuwafundisha walimu matumizi ya teknolojia pekee, bali pia kuwasaidia kuboresha mbinu za kufundisha, kuongeza ufanisi wa masomo na kutafuta njia mpya za kuwavutia wanafunzi.
“Lengo ni kuwawezesha walimu kuendana na maendeleo ya teknolojia, kutumia mbinu bora za ufundishaji na kugundua njia mpya za kuwashirikisha na kuwahamasisha wanafunzi,” alisema Prof. Fleischmann.

Mafunzo hayo yanahusisha maeneo sita ya kitaaluma ambayo ni Kiingereza, Biolojia, Hisabati, Ubunifu wa Nguo (Textile Design), Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT), pamoja na Ufundishaji wa Wazi na Shirikishi (Open and Blended Learning).
AI imepewa nafasi muhimu katika mafunzo hayo, huku walimu wakijifunza namna ya kutumia teknolojia hiyo na zana nyingine za kidijitali katika kutafuta taarifa, kuandaa masomo, kutengeneza nyenzo za kufundishia na kuwashirikisha wanafunzi.
Simu janja: Darasa linalobebwa mfukoni
Kwa mujibu wa Prof Fleischmann, mafunzo hayo yamezingatia pia changamoto za shule ambazo hazina maabara kubwa za kompyuta.
Alisema hali hiyo isiwe kikwazo kwa walimu kutumia teknolojia, kwa kuwa simu janja zinazopatikana kwa walimu na wanafunzi zinaweza kuwa nyenzo muhimu ya kujifunzia.
“Katika shule yenye kompyuta chache, mara nyingi walimu wana simu janja. Tunawafundisha namna ya kutumia vifaa hivyo kwa ufanisi ili kuboresha mchakato wa ujifunzaji,” alisema.
Mtazamo huo unaweka mkazo kwenye kutumia teknolojia ambayo tayari ipo, badala ya kusubiri shule ziwe na vifaa vya gharama kubwa.
“Msipobadilika, mtakuwa hamna nafasi”
Akifungua mafunzo hayo, Afisa Elimu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Abel Mtupwa, aliwataka walimu kutambua kasi ambayo teknolojia inabadilisha maisha ya wanafunzi wao.
Alisema wanafunzi wengi sasa wana uelewa mkubwa wa matumizi ya simu, mitandao ya kijamii, programu mbalimbali na AI, jambo linaloweka wajibu kwa walimu kuendelea kujifunza.
“Wanafunzi wenu wako mbele yenu katika matumizi ya teknolojia zinazochipuka kama programu za simu, mitandao ya kijamii, akili bandia na hata kompyuta, lakini baadhi yenu hamjui chochote,” alisema.
Mtupwa aliwataka walimu wasione teknolojia kama mpinzani wa taaluma yao, bali kama fursa ya kuimarisha uwezo wao na kuboresha matokeo ya wanafunzi.
Alitoa tahadhari kuwa kutokubali kujifunza na kuendana na mabadiliko hayo kunaweza kuwafanya walimu kupoteza ufanisi wao katika miaka ijayo.
“Msipokuwa makini, baada ya miaka michache mtakuwa hamna nafasi katika mazingira haya,” alisisitiza.
Mafunzo hayo yamewafikia walimu zaidi ya 1,700 na ni sehemu ya mpango wa “Teaching and Learning with Digital Resources, Tanzania”, ambao umeendelea tangu mwaka 2014.

Katika kipindi hicho, jumla ya walimu 1,710 kutoka mikoa ya Kilimanjaro na Arusha wamewahi kushiriki mafunzo hayo, wakiwakilisha zaidi ya shule 400 za sekondari.
Mafunzo kuzaa matokeo nje ya darasa
Mafanikio ya mpango huo yanaonekana pia kupitia walimu walioshiriki mafunzo katika miaka iliyopita.
Mark Lyimo, mwalimu wa Shule ya Sekondari Mboni iliyopo Kata ya Mamba, Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, anasema mafunzo ya mwaka jana yalimsaidia kuondokana na hofu aliyokuwa nayo kuhusu matumizi ya teknolojia.
Anasema sasa ana kujiamini zaidi katika kutumia teknolojia zinazoibuka katika ufundishaji na ujifunzaji, huku akitumia ujuzi huo kutengeneza nyenzo zenye vielelezo na kuboresha ufundishaji.
Ujuzi huo pia ulimwezesha kuanzisha kundi la mtandaoni linalowakutanisha walimu na wazazi au walezi kwa ajili ya mawasiliano kuhusu maendeleo ya wanafunzi.
Kutoka mafunzo hadi darasa la ushonaji
Kwa mwalimu Holiness Kaduma wa Shule ya Sekondari Mpirani, Manispaa ya Moshi, mafunzo hayo yalizaa wazo lililogeuka kuwa fursa ya ujuzi kwa wanafunzi.
Baada ya kushiriki mafunzo mwaka jana, Kaduma alianzisha darasa la Textile Design shuleni hapo ambalo kwa sasa lina wasichana 15.
Kupitia juhudi zake, aliomba msaada kutoka kwa wadau na kupata mashine tano za kushonea, hivyo kuwawezesha wanafunzi kujifunza ujuzi wa vitendo.

“Baada ya mafunzo ya mwaka jana, niliweza kuomba msaada na kupata mashine tano za kushonea. Sasa wasichana 15 wanajifunza ujuzi wa vitendo ambao naamini utakuwa na manufaa katika maisha na taaluma zao za baadaye,” alisema.
Ingawa Textile Design bado haifundishwi kama somo la mtihani katika ngazi ya Ordinary Level katika shule hiyo, juhudi zinaendelea kuhakikisha somo hilo linapata nafasi katika elimu ya ufundi na vitendo.
SMMUCo ikiingia zaidi kwenye teknolojia za kizazi kipya
Mafunzo hayo yanafanyika wakati SMMUCo yenyewe ikijielekeza zaidi kwenye taaluma zinazohusiana na teknolojia za kizazi kipya.
Hali hiyo inaifanya nafasi ya SMMUCo katika mafunzo ya walimu na matumizi ya teknolojia kuwa sehemu ya mwelekeo mpana wa chuo katika kuandaa wataalamu wanaokabiliana na mahitaji ya uchumi na jamii ya kidijitali.
Mwalimu wa kesho si chanzo pekee cha taarifa
Mabadiliko haya yanaendelea kubadili pia nafasi ya mwalimu darasani. Mwanafunzi wa sasa anaweza kupata taarifa nyingi kupitia simu na intaneti hata kabla hajakutana na mwalimu.
Hivyo, jukumu la mwalimu linazidi kuhamia katika kumsaidia mwanafunzi kuchambua taarifa, kutofautisha taarifa sahihi na zisizo sahihi, kuelewa maarifa na kuyatumia kwa njia yenye manufaa.
Kwa maana hiyo, teknolojia haiwezi kuchukua nafasi ya mwalimu, lakini mwalimu anayejua kuitumia anaweza kuwa na uwezo mkubwa zaidi wa kuwafikia, kuwashirikisha na kuwaandaa wanafunzi kwa dunia inayobadilika kwa kasi.

Kwa walimu 215 wanaopitia mafunzo Moshi, ujumbe wa msingi si kwamba teknolojia inakuja darasani. Teknolojia tayari ipo darasani; kinachobadilika sasa ni uwezo wa mwalimu kuitumia.
Wawezeshaji wa mafunzo hayo ni Prof Karl Fleischmann, Profesa mstaafu wa Sayansi ya Mazingira, Chuo Kikuu cha Seychelles, Edith Müller, Mhadhiri, Chuo Kikuu cha Elimu ya Ualimu Zurich (PHZH), Uswisi na Christian Bwaya wa Chuo Kikuu cha Dodoma.
Wengine ni Markus Honegger — Mwalimu wa Lugha za Kisasa, Uswisi, Happiness Maleko — Chuo Kikuu cha Kilimo na Teknolojia cha Mwalimu Nyerere, Dk Maranya Mayengo — Mhadhiri Mwandamizi, Nelson Mandela African Institution of Science and Technology (NM-AIST), Arusha,, Ernst Elsener — Mkuu mstaafu wa Idara ya Didactics of Informatics katika Chuo Kikuu cha Elimu ya Ualimu, Uswisi na Isaki Awaki Ara — Mwalimu, Shule ya Sekondari ya Mawenzi, Moshi, Kilimanjaro.



