TAASISI ya Hakika Tunajifunza kwa kushirikiana na Kampuni ya Ushauri wa Kitaalamu ya GJS, wameandaa kampeni maalum ya kutoa elimu ya mazingira na afya kwa wanafunzi wa shule za sekondari nchini.
Kampeni hiyo itakayoenda sambamba na ufanyaji wa mazoezi ya viungo, inatarajiwa kufanyika Septemba 10, mwaka huu katika shule ya Sekondari Makurumla iliyopo jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa Kampeni ya Hakika Tunajifunza, Furaha Mbakile, amesema kampeni hiyo, itasaidia kuongeza idadi ya wanafunzi wafanyao mazoezi ya kujenga mwili, pamoja na kupata elimu hiyo ya mazingira na afya.
Amesema kampeni hiyo itafanyika katika shule mbalimbali zilizopo kwenye wilaya tano za Dar es Salaam.
“Kampeni hii ilizinduliwa rasmi Julai 27, 2022 ina lengo la kwenda sambamba na Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye anakauli mbiu yake ya kutaka kazi kuendelea, hivyo na sisi tunataka wanafunzi waendelee kujifunza,” amesema
Naye Mkurugenzi Mtendaji Kampuni ya Ushauri wa Kitaalamu ya GJS, Mchungaji mstaafu Joseph Chaggama, amesema watashirikiana na wadau mbalimbali pamoja na serikali kufanikisha kampeni hiyo.