Waonywa kugawa mashamba pori yaliyofutwa

Waonywa kugawa mashamba pori yaliyofutwa

MKUU wa Mkoa wa Morogoro, Fatma Mwasa, amewaonya wataalamu wa ardhi wa mkoa huo kuacha mpango wa kugawa kwa wawekezaji wengine ardhi ya mashamba pori 11, ambayo yamefutwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Mwasa alitoa angalizo hilo alipopata fursa ya kutoa salam za serikali ya mkoa katika kikao maalumu wa Halmashauri Kuu ya Chama  Cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Morogoro.

Alisema kwenye utendaji kazi, amejielekeza katika maeneo makubwa matano, yakiwemo ya huduma za jamii, ambapo atatumia muda mwingi , nguvu na maarifa mengi na wataalamu wa kutosha, ili kutatua changamoto mbalimbali za wananchi zikiwemo za migogoro ya ardhi.

Advertisement

Alisema Rais alishafuta mashamba pori 11 yaliyopo katika  baadhi ya halmashauri za wilaya za mkoa huo, lakini katika amebaini wataalamu wa ardhi wameshakuwa na mipango mingine ya wawekezaji.

“ Naomba niwaambie wataalamu wa ardhi ya kwamba ardhi iliyofutwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, itakwenda kwa wakulima wanyonge, wadogo na si kwa wawekezaji, kwani wawekezaji  wa sasa ni wananchi wenyewe,” alisema Mwasa.

Pia alisema yapo maeneo mengine yaliyotengwa kwa ajili ya wafugaji, ambako hakutakuwa na  shughuli za kilimo, lengo ni kuondoa migogoro ya wakulima na wafugaji.

“ Watu wengi wanazungumzia migogoro  ya ardhi, lakini hatujakaa chini  kuilijadili, hivyo nawaomba wabunge wa mkoa wetu, wenyeviti wa halmashauri  na viongozi wa chama tukae pamoja, ili tupate maelezo kwa nini migogoro ni mingi Morogoro,“ alisema Mwasa.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa chama hicho mkoa, Dorothy Mwamsiku, alimshukuru Rais kwa kutoa fedha nyingi kwa mkoa huo, kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbambali ya maendeleo kwa wananchi.