WANACHAMA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wametakiwa kuchagua viongozi kwa kuzingatia sifa za mwombaji.
Kauli hiyo ilitolewa na Msimamizi wa Uchaguzi wa viongozi wa Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT) Wilaya ya Tanga, Kumotola Kumotola ambaye alisema misingi ya chama hicho ni usawa na umoja.
“Tukianza kuchagua kwa misingi ya vimemo (maelekezo mahususi) na wenye nacho hatutaweza kupata viongozi ambao ni waadilifu ambao wataweza kukipigania chama kwenye chaguzi zinazokuja,” alisema Kumotola.
Aidha, alisema dhana ya mtu mmoja kuwa na vyeo vingi ndani ya chama nayo kwa sasa imepitwa na wakati kwa kuwa CCM ni chama kikubwa na kina watu wengi wenye uwezo wa kukitumikia.
Mkurugenzi wa Uchaguzi Wilaya ya Tanga, Twalib Berege aliwataka ambao wameshindwa katika uchaguzi huo kutotengeneza makundi ambayo yatasababisha mpasuko.
Mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Tanga, Moza Shilingi aliwataka wanawake ndani ya CCM wawe na umoja ili waweze kujiletea maendeleo.
“Niwaombe wanawake wenzangu tujitokeze kugombea nafasi za uongozi katika nyadhifa mbalimbali ili kuhakikisha Jimbo la Tanga na kata zote hazipotei na wala mpinzani hatii mguu ili kuifanya CCM iendelee kushika dola,” alisema.
Katika uchaguzi huo Shilingi alishinda kwa kura 344 dhidi ya mpinzani wake, Jane Hova aliyepata kura 23.