MTANDAO wa Wabunge wa Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (PNoWB), wameridhishwa na jinsi wanufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini (TASAF) ulivyoweza kubadilisha maisha yao.
Pia wameguswa na jinsi wanufaika wa Tasaf wanavyoweza kutumia kiasi kidogo cha fedha kujikimu pamoja na gharama kubwa za maisha.
Wanachama wa mtandao huo, wakiwemo wa tawi jipya la Tanzania pamoja na mambo mengine wametembelea miradi inayotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii – Tasaf katika Kijiji cha Ikombolinga wilayani Chamwino mkoani Dodoma.
Mwenyekiti wa mtandao huo na Mbunge wa Birmingham Hodge Hill, Liam Byrne alisema dunia nzima inaweza kuja na kujifunza kutokana na jinsi Serikali ya Tanzania inavyobadilisha maisha ya wananchi maskini.
Byrne, ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Fedha wa Uingereza alisema amebahatika kuona kazi kubwa ambayo walengwa wanafanya kujijenga wenyewe na Taifa kwa ujumla.
Mwenyekiti wa Mtandao huo tawi la Tanzania, Neema Lugangira alisema: “Tumefurahi kuwa hapa na tumeshuhudia kazi nzuri ambayo serikali inafanya kwa msaada kutoka kwa wafadhili.”
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Tasaf, Ladislaus Mwamanga alisema kuwa kwa miaka mingi, mpango huo umechangia ukuaji wa uchumi wa nchi katika sekta nyingi.
Naye mmoja wa walengwa, Margaret Puma (68) alieleza maisha yake ya awali kabla hajaingia katika Mpango na kusimulia jinsi alivyoanza kutumia ruzuku yake ya kwanza kwa kukodi shamba na kuanza kilimo cha alizeti ambacho kilimpatia fedha ya kutosha kujenga nyumba ya bati na kununua mifugo.