Yanga yatupa dongo kwa mtani

YANGA imetupa dongo kwa watani zake wa Jadi Simba wakisema hakuna wa kuwazuia kucheza kwenye Uwanja wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni (KMC).

Kauli hiyo inakuja baada ya Yanga kucheza kwa mara ya kwanza kwenye uwanja huo mchezo wa kirafiki dhidi ya Kiluvya juzi na kupata ushindi wa mabao 3-0.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam Leo Msemaji wa Yanga Ally Kamwe amesema baada ya kuutumia uwanja huo kumezuka maneno kwenye mitandao kwamba wamewafuata watani zao Simba ambao wamekuwa wakiutumia kama uwanja wa nyumbani kwenye mechi za Ligi Kuu.

Pia, Uwanja huo umekuwa ukitumiwa na timu ya KMC kama uwanja wake wa nyumbani.

“Uwanja wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni umejengwa kwa pesa zetu. Pale KMC panapataje heshima kama Yanga wasipoenda, tumenogewa na tutarudi tena, kama imewauma hameni,”amesema Kamwe.

SOMA: Yanga yakana kudaiwa, vifaa vipya hadharani

Baada ya mchezo huo, Kamwe amesema wanatarajia kucheza mchezo mwingine wa kirafiki hivi karibuni mbele ya mashabiki.

Amesema licha ya wachezaji 14 kwenda kuzitumikia timu zao za taifa, waliobaki 13, wawili ni majeruhi ambao ni Farid Mussa na Yao Attohoulla na wengine 11 ndio wazima.

SOMA: Kamwe: Tutachukua hatua kunyimwa goli jana

Kamwe amesema wachezaji hao 11 waliongezewa nguvu na wachezaji watatu kutoka kikosi cha vijana chini ya umri wa miaka 20 na kusaidia timu kushinda mchezo wa kwanza wa kirafiki.

“Tunafikiria kucheza mechi nyingine ya mazoezi mbele ya mashabiki kwa ajili ya kukiimarisha kikosi chetu kujiandaa na ligi na mashindano ya kimataifa,”amesema.

Habari Zifananazo

Back to top button