Inua 1961 kuandaa kizazi cha wavumbuzi Afrika

DAR ES SALAAM: Vijana nchini Tanzania wanatarajiwa kupata fursa mpya za kuendeleza vipaji vyao (Schoolarship) katika sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati (STEM), baada ya Taasisi ya Inua Hub kuzindua mpango wa muda mrefu wa Inua 1961 unaolenga kuwaandaa vijana kwa fursa za elimu, ajira, ujasiriamali na uongozi kimataifa.
Mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji wa Inua Hub, Johnas Chami, amesema mpango huo unalenga kujenga kizazi cha wavumbuzi wa Afrika kitakachotumia teknolojia kutatua changamoto mbalimbali na kushindana katika uchumi wa kidijitali duniani.

Mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji wa Inua Hub, Johnas Chami, akizungumza wakati wa kuwasilisha taarifa ya uzinduzi wa Inua 1961 jijini Dar es Salaam jana.
Amesema Inua 1961 hautajikita katika kutoa ufadhili wa masomo pekee, bali jukwaa la kuwapatia vijana fursa mbalimbali ikiwemo programu za kubadilishana wanafunzi, mafunzo kwa vitendo, utafiti, maendeleo ya ujuzi wa kidijitali, akili bandia (AI), uongozi na ujasiriamali.

Washiriki kutoka taasisi mbalimbali wakifuatilia na kusikiliza taarifa ya uzinduzi wa Inua 1961 Dar es Salaam jana.
“Tunataka vijana waweze kufikia fursa za kimataifa, kuunganishwa na kampuni za nje kwa ajili ya ajira, lakini pia wawe na uwezo wa kujiajiri kupitia ubunifu na uanzishaji wa biashara,” alisema Chami.
Alisema uamuzi wa kuanzisha mpango huo umetokana na kubaini kuwa kuna vipaji vingi miongoni mwa vijana, lakini nafasi za kuviendeleza bado ni chache, huku baadhi yao wakikosa ujuzi unaohitajika wanapomaliza vyuo vikuu.

Washiriki kutoka taasisi mbalimbali wakifuatilia na kusikiliza taarifa ya uzinduzi wa Inua 1961 Dar es Salaam jana.
Kwa mujibu wa Chami, vijana wenye vipaji watapatikana kupitia shule, vyuo vikuu, jamii na kambi maalumu za mafunzo zitakazoandaliwa kwa ajili ya kuwabaini na kuwaendeleza.
Alisema mpango huo utazingatia pia kuwawezesha wanawake ambapo asilimia 60 ya washiriki wanatarajiwa kuwa wanawake na asilimia 40 wanaume, hatua inayolenga kuongeza ushiriki wa wanawake katika masomo na taaluma za sayansi na teknolojia.
“Tumelenga kuwapa wanawake nafasi zaidi kwa sababu katika maeneo ya sayansi na teknolojia bado idadi yao ni ndogo. Tunataka kuhakikisha wanapata mazingira bora ya kukuza uwezo wao,” alisema.

Mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji wa Inua Hub, Johnas Chami, akizungumza mbele ya washiriki wakati wa kuwasilisha taarifa ya uzinduzi wa Inua 1961 jijini Dar es Salaam jana.
Chami alieleza kuwa awamu ya kwanza ya utekelezaji wa Inua 1961 itaanza Tanzania kuanzia mwaka 2027 hadi 2030, kabla ya kupanuliwa katika nchi za Afrika Mashariki kuanzia mwaka 2031 hadi 2035, zikiwemo Kenya, Uganda, Zambia na Rwanda.
Awamu ya tatu ya mpango huo inalenga kufikia bara zima la Afrika kuanzia mwaka 2036 hadi 2045, kwa lengo la kuibua na kuunganisha vipaji vya vijana wa Afrika na fursa za kimataifa.

Aidha, Taasisi ya Inua Hub imepanga kufanya ziara katika mikoa mbalimbali ya Tanzania kwa ajili ya kusaka vipaji na kuwafikia vijana wenye ndoto za kubadilisha maisha yao kupitia elimu, teknolojia na ubunifu.

Mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji wa Inua Hub, Johnas Chami, ( wakwanza kushoto) akiwa na Ofisa wa Kitengo cha Ushirikiano na Mahusiano ya Nje wa Inua Hub, Farida Rashidi ( wapili kutoka kushoto) na baadhi ya viongozi wengine wa Inua Hub mara baada ya uzinduzi wa Inua 1961.
Chami alisema vijana wengi wana ndoto za kusoma nje ya nchi au kupata nafasi za kimataifa, lakini changamoto za kifedha na ukosefu wa taarifa zimekuwa kikwazo, jambo ambalo Inua 1961 inalenga kulitatua kwa kuwafungulia milango ya fursa.




