Mikopo ya vijana yaonyesha matokeo

SERIKALI kupitia Ofisi ya Rais Maendeleo ya Vijana inaendelea kutekeleza Programu ya Mikopo ya shilingi bilioni 200 inayolenga kuwawezesha vijana kuanzisha, kukuza na kupanua shughuli za kiuchumi katika maeneo mbalimbali nchini.
Utekelezaji wa programu hiyo umeanza kuonyesha matokeo huku vikundi vya vijana vikinufaika na mikopo na vifaa vya uzalishaji vinavyowawezesha kuongeza tija, kupanua biashara na kufungua fursa za ajira. SOMA: Sh bilioni 1.88 yanufaisha miradi 85 ya vijana
Jijini Arusha, Serikali imetoa shilingi milioni 730 kwa vikundi vya vijana vinavyojishughulisha na uzalishaji wa chakula, utengenezaji wa chaki na dawa zinazotokana na mimea.Fedha hizo zinatarajiwa kusaidia kuongeza uzalishaji na kuimarisha shughuli za kiuchumi za vikundi hivyo.
Katika Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya, vikundi vya vijana vilikabidhiwa shilingi milioni 349 kwa ajili ya kuendeleza kilimo cha kisasa na kuongeza uzalishaji wa mazao, hatua inayolenga kukuza kipato na kuchangia maendeleo ya uchumi wa eneo hilo.
Wilayani Kyela, Mkoa wa Mbeya, vikundi vya vijana wanaojishughulisha na huduma za usafiri wa bodaboda vilipokea pikipiki 22 zenye thamani ya shilingi milioni 87 kupitia programu hiyo. Hatua hiyo inatarajiwa kuongeza uwezo wa vijana hao kujiajiri na kuboresha kipato chao.
Huku Wilaya ya Ludewa mkoani Njombe imenufaika na mradi wa kisasa wa ufugaji wa samaki kwa vizimba wenye thamani ya shilingi milioni 400. Mradi huo unatarajiwa kuongeza uzalishaji wa samaki, kufungua fursa za ajira na kuimarisha uchumi wa vijana wanaoshiriki katika shughuli hiyo.
Utekelezaji wa Programu ya Mikopo ya shilingi bilioni 200 ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuwawezesha vijana kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji, kuongeza ajira na kukuza uchumi kupitia uwekezaji katika miradi ya maendeleo.



