Benki yatumia parokia kama mawakala wa kimkakati

MAWAKALA 28 kati ya 1,957 wa Benki ya Biashara ya Mkombozi ni mawakala wa kimkakati waliopo katika maeneo maalumu ya parokia au taasisi za kanisa ambazo ni sehemu muhimu ya soko mkakati la benki; Imefahamika.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Biashara ya Mkombozi, Respige Kimati amebainisha hayo katika Mkutano Mkuu wa 17 wa Wanahisa wa benki hiyo uliofanyika Dar es Salaam wakati akitoa taarifa yake kwa wanahisa kuhusu utendaji wa benki kwa mwaka 2025.
“Mtandao wa mawakala wa kibenki uliongezeka kwa asilimia 42 na mawakala 1,957 kutoka 1,377 mwaka 2024 na kati yao, 28 ni mawakala wa kimkakati waliopo maeneo maalumu ya parokia au taasisi za Kanisa…,” amesema.
Aidha, alisema benki hiyo inaendelea kupanua uwepo wake katika mikoa muhimu ya kiuchumi kwa kufungua matawi mapya kama vile Geita mwezi Novemba 2025 na Kahama mwezi Mei 2026 pamoja na kituo cha huduma za kibenki kilichopo Bagamoyo Juni 2026.
Akaongeza: “Uwekezaji huu unaendana na mkakati wa kuimarisha ukuaji wa biashara na faida endelevu.”
Kwa mujibu wa Kimati, ili wanahisa wanufaike zaidi na uwekezaji unaofanyika, hawana budi kujitokeza na kuongeza bidii kuwekeza katika hisa na kutumia huduma na bidhaa mbalimbali za benki hiyo.
Alisema kwa tathmini yao, asilimia 9.7 pekee ya wanahisa zaidi ya 16,000 (sawa na wanahisa 1,552) ndio wanaotumia huduma za benki hiyo jambo linalowakosesha fursa nyingi.
Katika mkutano huo mbele ya wanahisa, benki hiyo imefafanua uamuzi wake kupandisha kiasi cha gawio kwa wanahisa kutoka Sh 92.40 mwaka 2024 hadi Sh 100 kwa kila hisa.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya Mkombozi, Gasper Njuu amesema ongezeko hilo la gawio kwa kila hisa ni matokeo chanya ya kukua kwa faida za hisa, kukua kwa mtaji wa wanahisa pamoja na lengo la kuboresha maslahi ya wanahisa.
Amesema: “Wanahisa wamepokea kwa furaha pendekezo la bodi la kutoa gawio la Shilingi 100 kwa kila hisa tofauti na mwaka juzi lilipokuwa Shilingi 92.40 na hii ni kutokana na kuendelea kukua kwa biashara ya benki na ukubwa faida”.
Ameongeza: “Hata hivyo kutokana na dira na mwelekeo wa Benki ya Mkombozi, tunajiona hatujafikia hata asilimia 10 ya soko la benki yetu…”
Mjumbe wa Bodi ya Wakrugenzi wa Benki hiyo ambaye pia ni Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma, Askofu Mkuu Beatus KInyaiya amesema Mkombozi inalenga kuhakikisha inapata faida kupitia shughuli zake za kiadilifu ili kuwezesha ongezeko la gawio kwa wanahisa.
“Wawekezaji wanapowekeza fedha zao wanachokingoja ni faida kupitia gawio hivyo, wanahisa wanategemea ongezeko zaidi la hisa na kupata gawio kubwa zaidi,” amesema Kinyaiya.
Awali katika muhtasari wa utendaji wa benki kwa mwaka 2025 mbele ya wanahisa, Kimati amesema faida ya benki hiyo kabla ya kodi iliongezeka kwa asilimia 48 na kufikia Sh bilioni 17 kutoka Sh bilioni 11.49 mwaka 2024 kutokana na kuongezeka kwa mapato ya benki pamoja, kudhibiti na kupunguza gharama.
“Faida za hisa kwa wanahisa iliongezeka kwa asilimia 34 kutoka asilimia 29 mwaka 2024 huku mtaji wa wanahisa pia ukikua kwa asilimia 23 na kufikia Sh bilioni 49 kutoka Sh bilioni 40 mwaka 2024,” amesema Kimati.



