Unyanyapaa,vikwazo vilivyowafanya Joan,lissa kupigania ndoto zao

“WALINIAMBIA sitafika mbali. Wengine walisema bora nipewe mtaji niuze machungwa kuliko kuendelea kuota ndoto za kurudi shule.”
Hayo ni maneno ambayo Lissa Davis hawezi kuyafuta akilini. Alikuwa mwanafunzi wa kidato cha pili alipopata ujauzito, tukio lililobadilisha maisha yake kwa ghafla na ndoto ya kumaliza elimu ilionekana kufutika, huku jamii ikimhukumu kabla hata hajapata nafasi ya kujitetea.
Baada ya kugundulika kuwa ni mjamzito, wazazi wake walipitia maumivu makubwa ambapo mama yake aliamua kumpeleka kwa bibi yake eneo la Makumbusho jijini Dar es Salaam ili kumuepusha na macho na maneno ya watu waliokuwa wakiamini kuwa ameiangusha familia.
Hata hivyo kila alipotamani kuzungumzia kurejea shuleni, alikutana na kejeli na hukumu nyingi za kukatisha tamaa. “Watu walikuwa wakisema sasa nitakuwa wa kuzaa watoto tu, kwamba sitaweza tena kusoma wala kufanikiwa maishani,” anasema Lissa.
Lakini katikati ya maumivu hayo kulikuwa na mtu mmoja ambaye hakukubali ndoto za binti yake zife. Mama yake aliendelea kumtia moyo licha ya lawama nyingi alizokuwa akizipokea kutoka kwa ndugu na majirani. “Nilimwambia asisikilize maneno ya watu kwa sababu nilijua bado alikuwa na nafasi ya kubadilisha maisha yake,” anasema mama Lissa.
Mwaka 2022, Serikali ya Tanzania ilitangaza kuanza kutekeleza mpango wa kuwarejesha shuleni wasichana waliokatisha masomo, kutokana na tamko hilo Lissa alipata nafasi ya kujiunga na elimu ya sekondari kwa njia mbadala lakini bado safari hiyo haikuwa nyepesi.
Ilimbidi kumuacha mtoto wake akiwa na miezi 10 chini ya uangalizi wa mama yake ili aweze kurejea darasani. Aliishi mbali na mwanawe kwa kila wiki huku akitia bidi katika kusawazisha majukumu ya kuwa mama na wajibu wa kuwa mwanafunzi.
Alihakikisha kuwa alisoma kwa bidii na kufaulu mtihani wa kidato cha nne kwa daraja la pili, mafanikio yaliyowashangaza wengi waliokuwa wamekata tamaa naye. Baadaye alichaguliwa kujiunga na Kidato cha Tano katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Lugufu iliyo Mkoani Kigoma.

Mafanikio hayo yalibadili hata msimamo wa babu yake ambaye hapo awali alikuwa amesema hawezi kutumia fedha kumsomesha msichana aliyeshapata mtoto. “Baada ya kuona matokeo yangu, aliniambia atanilipia gharama zote za kidato cha tano na sita kama zawadi ya kufaulu,” anasema Lissa huku akitabasamu.
Leo hii ana ndoto ya kuwa mwanamitindo na anaamini hakuna kosa linalopaswa kumuondolea msichana haki ya kutimiza ndoto zake. Lakini wakati Lissa akianza kuona mwanga wa matumaini, kuna wasichana wengine ambao bado wanaendelea kupambana na changamoto zinazowafanya washindwe kabisa kutimiza ndoto zao.
Mmoja wao ni Joan Benard. Tofauti na Lissa, Joan alipata ujauzito akiwa bado mwanafunzi na baadaye akaishi pamoja na baba wa mtoto wake. Alipopata nafasi ya kurejea shuleni aliamini maisha yake yangebadilika, lakini changamoto mpya zilianza.
Baada ya kufaulu kidato cha nne kwa Daraja la Pili katika masomo ya sayansi, alipangiwa shule iliyokuwa mbali na nyumbani. Hakuwa na fedha za kujikimu, wala mtu wa kumsaidia kulea mtoto wake. “Nilikuwa nalia kila mara nilipokuwa shule . Nilijiona ni mkubwa kuliko wanafunzi wengine na hakuna aliyekuwa anaelewa ninachopitia maumivu ya kisakolojia yalizidi licha ya kujinyanyapaa niliona kama hisikajiki” anasema Joan.
Alijaribu kuomba uhamisho bila mafanikio akaamua kuacha shule. Ili kujikimu, alifanya kazi ya ukondakta wa asi huku akihifadhi ndoto yake ya kuendelea na elimu. Baadaye alipata nafasi ya kusoma kozi ya Health Records. Babu yake ambaye ndie mlezi pekee aliuza nguruwe ili kumlipia muhula wa kwanza Chuo, lakini baada ya mifugo kufa, uwezo wa familia uliishia hapo. Kanisa lilimsaidia muhula mmoja, kabla ya kusitisha ufadhili kutokana na sababu asizoelewa.
Kwa sasa Joan amesimamisha masomo, lakini bado anaamini siku moja atatimiza ndoto yake ya kuwa nesi. “Nimejifunza kujikubali. Naamini kila kitu kinawezekana. Wasichana wasikate tamaa ,” anasema Joan.
Mama wa Lissa anasema elimu inayotolewa bila ada ni msaada mkubwa, lakini haitoshi kwa wasichana wengi wanaorejea shuleni wakiwa tayari ni akina mama. Anasema wengi wanahitaji usafiri, chakula, malazi na sehemu salama za kuwaacha watoto wao wanapokuwa darasani. SOMA: Wasichana 13,000 warejea shuleni
“Wapo wanaoshindwa kuendelea si kwa sababu hawataki kusoma, bali hawana mtu wa kumwangalia mtoto au hawana nauli ya kwenda shuleni,” anasema. Hadithi za Lissa na Joan zinaonyesha kuwa kurudi shuleni ni mwanzo tu wa safari. Changamoto kubwa huanza baada ya kurejea darasani.

Unyanyapaa, umaskini, malezi ya watoto, msongo wa mawazo na ukosefu wa msaada kutoka kwa familia vinaendelea kuwa vikwazo vikubwa vinavyowafanya baadhi yao kushindwa kukamilisha masomo yao. Kwa Mujibu wa Taasisi ya Haki elimu takwimu za mwaka 2024 zinaonyesha ukubwa wa changamoto hiyo.
Haki Elimu ilisema sababu kubwa zinazowazuia kurejea ni pamoja na kukataliwa na baadhi ya wakuu wa shule kwa asilimia 29.4 ambapo, k atika baadhi ya maeneo, wakuu wa shule wamekuwa wakikataa kuwakaribisha tena wanafunzi waliojifungua, wakihofia kuathiri hadhi ya shule au kuleta “tabia mbaya” kwa wanafunzi wengine
Unyanyapaa ni asilimia 20.6 ambapo changamoto ya kisaikolojia ni kubwa kwa wasichana waliojifungua. Baada ya kupitia uzoefu mgumu wa kupata ujauzito na kujifungua wakiwa na umri mdogo, wasichana wengi hukosa ujasiri wa kurudi shule na kujumuika na wanafunzi wenzao.
Asilimia 17.7 ni ukosefu wa msaada wa kulea watoto , hofu ya kurudia makosa na asilimia 14.7 wengine wanajihisi kutengwa na kuhisi kuwa wakirudi shule watakutana na mazingira yale yale yaliyowafanya kupata ujauzito mwanzo. Hofu hii inawaondolea motisha ya kuendelea na masomo na hivyo kuishia kuacha shule kabisa. Na Umasikini kwa asilimia 11.8 ambapo inahusisha kugharamia watoto wao, gharama za ziada kama vile ada za shule, sare, na vifaa vya shule ni vigumu kumudu kwa familia maskini.
Katika kuhakikisha kuwa wanafunzi hao wanarudi shule kuendelea na masomo, serikali kupitia Wizara ya Elimu na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Ofisi ya Rais – TAMISEMI) walianzisha mradi wa kuwasaidia wasichana waliokatiza masomo kwa sababu mbalimbali kupata elimu bure.
Mradi huo ulianzishwa kupitia Taasisi ya Elimu wa Watu Wazima (TEWW) na kuitwa Mradi wa Kuimarisha Ubora wa Elimu ya Sekondari kwa Njia Mbadala. Kwa mujibu wa Mratibu wa mradi huo ,Baraka Kionywaki anasema mradi huo ulioanza mwaka 2022 ulilenga kuwarejesha wasichana 12,000 waliokatisha masomo kutokana na ujauzito na sababu nyingine.
Hata hivyo, hadi sasa wasichana 15,334 tayari wamerudishwa shuleni, idadi iliyovuka lengo la awali na Wizara ya Elimu, TAMISEMI na Benki ya Dunia.Kionywaki anasema awali kulikuwa na vituo 150 vya elimu ya sekondari kwa njia mbadala, lakini sasa vimeongezeka na kufikia 191 nchini kote ili kuwafikia wasichana wengi zaidi.
Anasema mbali na masomo ya kawaida, wanafunzi hupata mafunzo ya stadi za maisha, ujasiriamali, matumizi ya TEHAMA na ushauri wa kisaikolojia ili kuwasaidia kujenga upya maisha yao. Anasema mwaka huu pekee wanafunzi 401 wamefanikiwa kuchaguliwa kuendelea na kidato cha tano au vyuo vya kati, ishara kuwa mpango huo umeanza kuzaa matunda.
Kionywaki anasema katika vituo 14 vya mfano tayari kumeanzishwa sehemu za kulelea watoto, mabweni ya mama na mtoto pamoja na wahudumu wanaowatunza watoto wakati mama zao wakiwa madarasani. “Kituo cha Vijaliwa Vingi kilichopo Mlandizi Mkoani Pwani ni miongoni mwa vituo hivyo,”anasisitiza.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof Adolf Mkenda, anasema Serikali itaendelea kuhakikisha hakuna mtoto anayekosa haki ya kupata elimu, ikiwemo mabinti waliopata ujauzito, kama sehemu ya juhudi za kuimarisha usawa na ujumuishi katika sekta ya elimu nchini.
Prof Mkenda anasema kuwa serikali imeendelea kuiweka elimu miongoni mwa vipaumbele vyake vya maendeleo, sambamba na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayolenga kujenga jamii yenye maarifa na ujuzi. “Rais Samia Suluhu Hassan anasisitiza kuwa kila mtoto wa Kitanzania lazima apate elimu. Kwa msingi huo, Serikali imeweka mkazo katika kuhakikisha usawa na ujumuishi katika elimu kwa watoto wote,” anasema Prof Mkenda.
Anasisitiza,“Hakuna mtoto atakayeachwa nyuma katika mfumo wa elimu. Hata mabinti waliopata ujauzito wanaruhusiwa na wanapaswa kurejea shuleni kuendelea na masomo yao. Anasema wanaendelea kuboresha mazingira ya shule ili yawe salama na rafiki kwa watoto wote.
Kwa upande wake, Katibu wa Mtandao wa Wazee wa Mila Tanzania, Chifu Girihuida Gegasa Shulumbu, anasema jamii ina wajibu wa kubadili mtazamo wake na kuwasaidia wasichana walipata mimba shule badala ya kuwasema vibaya. Anasema badala ya kuwanyanyapaa wasichana waliopata ujauzito, jamii inapaswa kuwaunga mkono kwa sababu wengi wao bado wana uwezo wa kuwa wataalamu na viongozi wa kesho.
“Tumeshuhudia wanawake waliowahi kupitia changamoto hizo wakawa madaktari, walimu, manesi, wahandisi na viongozi.,” anasema. Mtazamo huo unaungwa mkono na mdau wa elimu kutoka HakiElimu, Florige Lyelu, anayesema sera ya kuwaruhusu wasichana kurejea shuleni imefungua ukurasa mpya wa haki ya elimu nchini.
Hata hivyo anashauri serikali na wadau kuongeza vituo vya kulelea watoto, huduma za ushauri nasaha na ufadhili wa mahitaji mengine ya elimu ili kuhakikisha wanaorejea shuleni hawakatishi tena masomo yao.



